Maghembe awatangazia kiama wanaotapeli watalii

Maghembe awatangazia kiama wanaotapeli watalii



Waziri wa Maliasili na Utalii,Profesa Jumanne Maghembe akikata utepe kuzindua jengo la maonesho na mikutano la Lake Nyasa Exhibition Hall katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha Arusha(AICC)jijini Arusha leo.Picha na Filbert Rweyemamu 

Arusha. Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe amesema atapambana na matapeli wote ambao wamekuwa wakiuza safari za watalii kwa njia ya mtandao.


Amesema kumekuwepo na malalamiko yanatolewa na baadhi ya watalii kuwa wanalipia huduma zote, lakini wanapofika nchini kwa ajili ya utalii hawakutani na waliowalipa fedha hizo.


Ameyasema hayo leo Alhamisi, Julai 20, wakati akizungumza katika ufunguzi wa jengo jipya la Lake Nyasa lililopo chini ya ukumbi wa mikutano wa AICC mjini hapa.


Amesema atahakikisha anawashughulikia wale wote wanaofanya utapeli huo kwenye mitandao kwani wamekuwa wakiitia aibu nchi.


"Kwa kweli hii ni aibu kubwa na utapeli huu umeshamiri kwa kiasi kikubwa na mwisho wa siku watasababisha tukose watalii, tunaomba sana hata wananchi watoe ushirikiano kuwafichua maana wengine nyie mnawajua pia, " amesema Maghembe.


Pia, Maghembe ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi wote wanaoingiza mifugo hifadhini kuacha mara moja kwani wanasababisha usumbufu mkubwa kwa watalii pindi mifugo hiyo inapokatiza maeneo ya hifadhi.


Naye, Mwenyekiti wa bodi ya AICC, Ladislaus Komba alisema kuwa kuwepo kwa ukumbi huo kutasaidia kuongeza kasi ya maendeleo kwa Jiji la Arusha na hata wajasiriamali kutokana na kuwa na eneo maalumu la kuonyesha bidhaa zao.


Komba amesema kuwa taasisi hiyo imejipanga kuhakikisha inaleta maendeleo kwa wakazi wa Arusha ambapo ina mpango wa kujenga kitega uchumi kingine cha ukumbi wa mikutano wa maonyesho jijini Arusha cha Mount Kilimanjaro.





Kwa upande wa Mkurugenzi wa AICC, Elishilia Kaaya amesema kuwa jengo hilo limegharimu kiasi cha Sh3.2 bilioni na kwamba uwepo wake utasaidia kuondoa changamoto mbalimbali za ukosefu wa eneo la kufanyia maonyesho.


















Post a Comment

0 Comments