Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu Tanzania imelaani waumini 10 wa dini hiyo kutekwa wakiwa katika msikiti wa Ali Mchumo wilayani Kilwa na sasa hawajulikani walipo.
Akizungumza leo Alhamisi Julai 27, Katibu wa jumuiya hiyo, Sheikh Ponda Issa Ponda amesema Julai 21, mwaka huu usiku waumini hao wakiwa wanasali katika msikiti huo walivamiwa na watu waliokuwa kwenye magari matano.
Amesema wavamizi hao waliingia msikitini na kuanza kuwapiga waumini hao kisha wakaondoka nao.
Amesema kabla ya kuingia msikitini, walipiga risasi sehemu mbalimbali za msikiti huo.
Ponda amesema wakati wakitekeleza unyama huo, majirani walisikia mayowe ya waumini hao.
Amesema baada ya hapo majirani walishuhudia wavamizi hao wakiwa wamewabeba waumini hao na kuwaingiza kwenye magari na kuondoka nao.
Amesema baada ya tukio hilo majirani walishuhudia damu nyingi ndani ya msikiti huo.
"Sijui kama watu hao watakuwa wazima hadi sasa kwa kuwa waliondoka wakiwa wamebebwa" amesema.
Amesema hadi sasa Polisi bado hawajatoa taarifa zozote kuhusiana na waumini hao.
0 Comments