YUSUSF MANJI TENA,SERIKALI YAKAMILISHA UPEPELEZI WA KESI YA DAWA ZA KULEVYA

YUSUSF MANJI TENA,SERIKALI YAKAMILISHA UPEPELEZI WA KESI YA DAWA ZA KULEVYA



Upande wa Jamhuri Umekamilisha upelelezi dhidi ya mfanyabiashara Yusuf Manji kuhusu tuhuma za Matumizi ya Dawa za Kulevya.Awali Wakili wa utetezi, Alex Mgongolwa alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha, kwamba mshtakiwa ni mgonjwa na amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili."Mheshimiwa mteja wangu ameshindwa kuja mahakamani kusikiliza kesi yake kwa sababu mgonjwa na amelazwa katika Hospitali ya Muhimbili," alidai Mgongolwa mahakamani hapo.
Kabla ya kutolewa taarifa ya ugonjwa wa mshtakiwa huyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Timon Vitalis, alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kwamba upande wa Jamhuri unaomba tarehe nyingine ya kusikiliza maelezo ya awali.
Hakimu Mkeha alisema kwa kuwa mshtakiwa ni mgonjwa, kesi hiyo itaanza kusikilizwa Agosti 10, mwaka huu.


Katika kesi ya msingi, Manji ambaye pia ni Diwani kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Mbagala Kuu jijini Dar es Salaam na mfanyabiashara maarufu nchini, anakabiliwa na mashtaka ya kutumia dawa za kulevya.


Ilidaiwa kuwa kati ya Februari 6 na 9 mwaka huu, eneo la Upanga Sea View jijini Dar es Salaam, Manji alitumia dawa za kulevya aina ya heroin.


Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana.


Hata hivyo, wakati Manji akiwa nje kwa dhamana katika kesi hiyo ya tuhuma za utumiaji dawa za kulevya, mfanyabiashara huyo alikosa dhamana juzi katika kesi nyingine inayohusiana na uhujumu uchumi.


Katika kesi hiyo ambayo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ilihamishia shughuli zake Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa Manji kwenye Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Manji na wenzake watatu walikosa dhamana baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha hati ya kuzuia dhamana kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akiomba washtakiwa wasipewe dhamana kwa usalama wao na maslahi ya taifa.


Pia DPP alieleza sababu nyingine ya Manji kunyimwa dhamana kuwa ni mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kushughulikia dhamana dhidi ya kesi hiyo. Washtakiwa wengine ni Ofisa Rasilimaliwatu Deogratias Kisinda (28), Mtunza Stoo, Abdallah Sangey (46) na Mtunza Stoo msaidizi, Thobias Fwele (43).


Ilidaiwa katika shtaka la kwanza kuwa Juni 30, mwaka huu eneo la Chang'ombe Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, Manji na wenzake walikutwa na askari polisi wakiwa na mabunda (majora) 35 ya vitambaa vinavyotengezea sare za JWTZ vyenye thamani ya Sh. milioni 192.5 na kwamba vilipatikana isivyo halali.


Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A' Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na askari polisi wakiwa na mabando nane ya sare za JWTZ zenye thamani ya Sh. milioni 44.


Upande huo wa Jamhuri uliendelea kudai kuwa, Juni 30, mwaka huu eneo la tukio la kwanza, washtakiwa walikutwa na mhuri wa JWTZ uliokuwa na maandishi 'Mkuu wa Kikosi 121 Kikosi cha Jeshi JWTZ' bila kuwa na uhalali, kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.


Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la tatu, washtakiwa wote kwa pamoja walikutwa na mhuri wenye maandishi "Kamanda Kikosi 834 KJ Makutupora Dodoma" bila uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.


Katika shtaka la tano, ilidaiwa siku ya tukio la tatu na la nne, mshtakiwa alikutwa na mhuri wenye maandishi "Comanding Officer 835 KJ Mgambo P.O BOX 224 Korogwe" bila kuwa na uhalali kitendo ambacho kinahatarisha usalama wa nchi.


Ilidaiwa katika shtaka la sita, Julai Mosi, mwaka huu eneo la Chang'ombe 'A', washtakiwa wote walikutwa na namba za gari zenye usajili wa SU 383 iliyopatikana isivyo halali.


Katika shtaka la saba, eneo la tukio la sita, washtakiwa walikutwa na namba za gari zenye namba ya usajili SM 8573 iliyopatikana isivyo halali.


Kwa mujibu wa mashtaka hayo yaliyofunguliwa chini ya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Usalama wa Taifa, washtakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao.


Hakimu Mkazi Huruma Shaidi alisema kesi hiyo itatajwa Julai 19 na washtakiwa watatu walipelekwa mahabusu ya Keko huku Manji akiwa chini ya ulinzi wa polisi wodini hapo.

Post a Comment

0 Comments