Serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma, PSSSF, kuanzia leo Agosti 1, mwaka huu huku sekta binafsi watasajiliwa katika mfuko wa NSSF, ambayo itatoa mafao na pensheni kwa wastaafu .
Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama, alisema, Serikali imekamilisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya matumizi ya mfuko wa PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko huo unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.
"Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF", alisema Mhagama.
Waziri Mhagama amesema kuwa Wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao zitaendelea kutolewa na mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile.
Akizungumzia rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa Waziri Mhagama amesema itahamishiwa katika Mfuko mpya wa PSSSF.
Pia Waziri Mhagama amewatoa hofu ya kupoteza ajira watumishi wote wa mifuko iliyounganishwa kwa kuwa watahamishiwa katika mfuko mpya ambako uongozi wa mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa taasisi.
Kabla ya PSSSF kuzaliwa kulikuwa na mifuko mitano ya aina hiyo ambayo ni NSSF, LAPF, GEPF, PPF na PSPF lakini serikali kwa kutumia sheria mpya imeipunguza mifuko hiyo na kuweka utaratibu wa mifuko miwili ambayo sasa ni NSSF unaoshughulikia watumishi wa sekta binafsi na PSSSF ambao wanachama wake ni watumishi wa sekta za umma.
Uundwaji wa PSSSF kama chombo kipya kwa watumishi wa umma ulitokana na kitendo cha Rais John Magufuli kusaini sheria namba 5 ya Mifuko ya hifadhi ya jamii mwaka 2018, iliyosainiwa mwezi Februari iliyotaka mifuko yote kuwa na mwangalizi mmoja ili kuboresha maslahi ya wastaafu.
0 Comments