Afisa wa Polisi adaiwa faini bilioni 1 kwa kumshika wakili wa Tundu Lissu

Afisa wa Polisi adaiwa faini bilioni 1 kwa kumshika wakili wa Tundu Lissu



Wakili Fatma Karume amefungua kesi ya madai akidai kulipwa fidia ya shilingi bilioni moja kutoka kwa Inspekta (mpelelezi) wa Polisi, Eugene Mwampondela wa Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es salaam.

Wakili Fatma anataka alipwe na mpelelezi huyo kiasi cha shilingi za kitanzania bilioni moja kwa makosa matatu ya kumuingilia mwilini mwake, kumbughudhi na kumzuia kufanya kazi yake (assault, battery, and misfeasance in public office).

Fatma amesema kuwa Inspekta Mwampondela alimshika na kumvuta mkono, hatua iliyomsababishia maumivu kwenye mkono wake.

“Ukiandika nalishtaki Jeshi la Polisi na wewe nitakufikisha mahakamani. Mimi nimemshtaki Inspekta Mwampondela kwa kosa la kuniingilia mwilini na kunivuta mkono.

“Aliniambia ameagizwa na wakubwa kutoka juu, hivyo namfikisha mahakamani amueleze Jaji huyo aliyemwagiza ni nani. Na mimi sitaki kushikwashikwa mwili wangu, kwahiyo nataka anilipe shilingi bilioni moja ili liwe fundisho kwa wengine,” alisema Fatma Karume.

Fatma alikutana na kadhia hiyo juzi alipokuwa katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam akiwa ni mmoja wa mawakili wa Mbunge wa Singida Mashariki ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Tundu Antipas Lissu.

Post a Comment

0 Comments