Polepole: Waache waondoke

Polepole: Waache waondoke


Wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea ndani ya CCM kuwapata viongozi wapya wa ngazi zote, wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Kata ya Kidatu mkoani Morogoro, wamejiuzulu kwa madai ya kushindwa kutimiza wajibu wao wa uongozi.


Wajumbe hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa kata hiyo, Magungu Alex waliachia ngazi muda wao wa uongozi wa miaka mitano ukiwa tayari umemalizika.


Kwa mujibu wa Katiba ya CCM, uchaguzi ndani ya chama hicho huwa unafanyika kila baada ya miaka mitano, waliojiuzulu waliingia madarakani mwaka 2012.


Katika taarifa ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole aliye kwenye ziara ya kuimarisha chama hicho na kukagua maendeleo ya uchaguzi, wajumbe hao waliachia ngazi baada ya kuwapo kwa malalamiko kutoka kwa wanachama kuwa wameshindwa kutekeleza wajibu wao, ikiwamo kutosimamia ipasavyo uchaguzi unaoendelea.


Polepole alisema sababu nyingine ya kujiuzulu kwao ni kushindwa kusimamia rasilimali za chama hicho, usaliti wakati na baada ya uchaguzi na tuhuma za kuisababishia kata hiyo ishindwe kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.


“Haipaswi wakati wowote kugeuza chama hiki kuwa chama cha viongozi, tangu awali msingi wa kuanzishwa kwake kiwe chama cha wanachama kinachoshughulikia shida za watu,” alisema.


Baadhi ya wanachama, walisema viongozi walioachia ngazi wamechelewa kufanya hivyo kwa sababu muda wa uongozi wao ulikuwa umeshamalizika. “Wamekisababishia hasara chama kwa miaka mitano yote walipokuwa madarakani, kwa sasa sioni kama wamejiuzulu ila muda wao umeisha,” mjumbe wa Halmashauri ya Kata ya Msewe wilayani Ubungo, Frank John.

















Post a Comment

0 Comments