Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuachia huru aliyekuwa Kamishna wa TRA, Tiagi Masamaki na Wenzake watano waliokuwa wakishtakiwa na makosa ya uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya sh. Bilioni 12.7.
Washtakiwa hao wameachiwa na Hakimu Mkazi Huruma Shahidi baada ya upande wa mashtaka uliokuwa ukiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi, Timon Vitalis kuiomba mahakama kufanya hivyo chini ya kifungu cha 91(1) ya makosa ya jinai (CPA) kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa hao.
"Mheshimiwa Hakimu kesi hii leo imekuja kwa ajili ya kutajwa, hata hivyo tuna maombi, DPP amewasilisha Nolle Prosque, hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi ya washtakiwa", amesema Wakili wa Serikali Timon Vitalis.
Hakimu Shahidi alikubaliana na ombi hilo na kuwaachia huru washtakiwa.
Mbali na Masamaki, washtakiwa wengine waliokuwa katika kesi hiyo iliyotokana na sakata la makontena 329 ni Meneja Kitengo cha Huduma za Ushuru TRA, Habib Mponezya (45) na Meneja Msimamizi na Ufuatiliaji wa Forodha, Burton Mponezya (51).
Msimamizi Mkuu Kitengo cha Ushuru wa Forodha ICD Azam, Eliachi Mrema (31), Mchambuzi Mwandamizi wa Masuala ya Biashara TRA, Hamis Omary (48), Meneja wa Oparesheni za Usalama na Ulinzi ICD, Raymond Adolf Louis (39) na Meneja wa Azam ICD, Ashrafu Khan (59) na Haroun Mpande (28) wa kitengo cha Mawasiliano ya Kompyuta ICT TRA.
Hata hivyo, DPP amewafutia mashtaka watuhumiwa watano tu ambao ni,Tiagi Masamaki, Eliachi Mrema, Habibu Mponezya, Burton Mponezya na Ashraf Khan.
Hata hivyo, Raymond Louis, Haruni Mpande na Khakis Ally Omari wameendelea kushikiliwa na kusomewa mashtaka mapya pamoja na watuhumiwa wapya, Khalid Yusuph Hassan na Benson Vitalis Malembo.
0 Comments