USAJILI: Rodriguez atua Ujerumani

USAJILI: Rodriguez atua Ujerumani


Kiungo mshambuliaji wa mabingwa wa La liga na klabu bingwa barani Ulaya, Real Madrid, James Rodriguez amejiunga na Bayern Munich kwa mkataba wa mkopo wa miaka miwili ambako anakwenda kuungana na kocha wake wa zamani, Mtaliano Carlo Ancelotti.


Kiungo mshambuliaji wa Real Madrid, James Rodriguez

Rodriguez atafanyiwa vipimo vya afya na vigogo hao wa Ujerumani kabla ya kukamilisha uhamisho wake kwenda Allianz Arena katika dili ambalo litagharimu hadi Pauni Milioni 40.

Bayern pia itakuwa na nafasi ya kumnunua moja kwa moja mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Colombia mwishoni mwa mkopo huo Juni 30, mwaka 2019.

Mkataba wa sasa wa mkopo unagharimu Pauni Milioni 9 na Pauni Milioni 31 nyingine zitaongezwa iwapo mwishowe watataka kumnunua moja kwa moja mchezaji huyo.

Mchezaji huyo atakuwa katika kikosi cha Bayern ambacho Jumapili jioni kitakwenda kwenye michuano ya siku 12 ya Audi Summer Tour nchi za China na Singapore.

Mwenyekiti wa Bayern, Karl-Heinz Rummenigge ameelezea furaha yake baada ya kumpata mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 akisema kwamba alikuwa chaguo kuu la Ancelotti katika dirisha hili.

Ancelotti na Rodriguez walifanya kazi pamoja Real Madrid baada ya mchezaji huyo kujiunga na timu hiyo kwa dau la Pauni Milioni 63 mwaka 2014.

Post a Comment

0 Comments