Waziri Lukuvi akesha ofisini kutatua kero za ardhi

Waziri Lukuvi akesha ofisini kutatua kero za ardhi


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. William Lukuvi usiku wa kuamkia jana alitumia takribani saa 20 kuanzia saa 2 asubuhi hadi saa tisa usiku kusikiliza wananchi 189 wenye matatizo ya kero za ardhi ofisini kwake.

Mhe. William Lukuvi

Kwa taarifa zilizothibitishwa na Ofisa Habari wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hassan Mabuye amesema Waziri Lukuvi alifanya hivyo baada ya wananchi wenye kero kugoma kutoka ofisini kwake wakitaka hadi kero zao zisikilizwe.

“Wananchi wengi wenye matatizo na kero za ardhi kutoka maeneo ya Bagamoyo, Kibaha, Mkuranga, Kibiti na Dar es Salaam kwa ujumla wametumia fursa hii ya kipekee ya kuonana na waziri mwenye dhamana ya ardhi na kumuelezea kero zao na hatimaye kupatiwa ufumbuzi papo hapo,”amesema Mabuye kwenye mahojiano yake na Gazeti la Habari Leo.

Hata hivyo Mabuye amesema Wananchi hao wamesifu utendaji kazi wa Waziri Lukuvi hususani kwa hatua ya kukutana nao ana kwa ana na kutatua kero zao za ardhi ambazo ni za muda mrefu huku akisema haijawahi kutokea hata siku moja Waziri kukesha ofisini.

Mwanzoni mwezi Juni 2017, Waziri Lukuvi alitoa tangazo la kuwataka wakazi wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, ambao wangependa kumuona, wafike katika ofisi yake ya Kanda ya Dar es Salaam iliyopo ghorofa ya pili, jengo la Wizara ya Ardhi – Magogoni, Kivukoni ili kujiandikisha majina yao, anuani na namba zao za simu.

Post a Comment

0 Comments