Bomoabomoa kusomba nyumba za ibada 30, vituo vya afya vitano Dar

Bomoabomoa kusomba nyumba za ibada 30, vituo vya afya vitano Dar


Mchungaji wa Kanisa la River Healing Ministry of Tanzania, John Kyashama akionyesha kanisa hilo lililopo Kibamba Luguruni jijini Dar es Salaam jana, ambalo ni moja ya nyumba za ibada zilizowekwa x kwa ajili ya kuvunjwa ili kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro. Picha na Salim Shao 
Kwa ufupi

Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) walisema muda wowote wanatarajia kuanza utekelezaji wa kubomoa nyumba zilizowekewa alama ya X katika barabara hiyo kwa madai kuwa tayari muda waliopewa wahusika kubomoa wenyewe umeshamalizika.
By Tumaini Msowoya na Jackline Masinde mwananchipapers@mwananchi.co.tz


Zaidi ya nyumba 30 za ibada, vituo vya mafuta sita, vituo vya afya vitano, kituo cha polisi na ofisi ya Kata ya Msigani jijini Dar es Salaam ni kati ya majengo yatakayobomolewa ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.


Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) walisema muda wowote wanatarajia kuanza utekelezaji wa kubomoa nyumba zilizowekewa alama ya X katika barabara hiyo kwa madai kuwa tayari muda waliopewa wahusika kubomoa wenyewe umeshamalizika.


Mwananchi ilifanya tathmini kuanzia eneo la Kimara hadi Kiluvya jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa makanisa 20 na misikiti 11 itakumbwa na bomoabomoa hiyo kikiwamo kituo cha maombi na maombezi cha Kanisa la Ufufuo na Uzima kinachomilikiwa na Askofu Josephat Gwajima kilichopo eneo la Mbezi Inn.


Makanisa mengine yatakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ni Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, KKKT Usharika wa Mbezi Luis, Roman Katholiki Kimara litakalobomolewa nusu, The River Hilling Ministry Of Tanzania la Kibamba, Anglikana Stop Over na Calvary Salvation Church lililopo Kibamba.


Makanisa mengine ni Kaprenan lililopo Kibamba, TAG - Suka, Pentekoste Of Tanzania Kiluvya, Nayoth Church Kiluvya, KLPT la Bwawani, Kapernan Centre Mbezi, TAG Carvary Tample Mbezi Inn, GRC Mbezi Inn na TAG Rejoice Center Mbezi.


Hata hivyo, baadhi ya makanisa yameshabomolewa kutii agizo la kubomoa kwa hiyari likiwamo la Moravian Kimara Stop Over na KKKT Kibamba ambako leo wanafanya ibada ya mwisho kabla ya kuhamia eneo jipya.


Misikiti itakayokumbwa na bomoabomoa hiyo ni Masjid Kilumbi Islamic Center - Kimara Mwisho, Dalul Mustafah wa Kimara Stop Over, Masjid Baitul Maamur, Masjid Jaaria, Masjid Baitul Maamur na Almasjid Nuur iliyopo Kiluvya.


Misikiti mingine ni Masjid Jaalia Gogan, Masjid Nuur Kibamba CCM.Pia immo misikiti mitatu ya Mbezi Inn, Mbezi Luis na Temboni.


Vituo vya mafuta vinavyotakiwa kubomolewa ni Henry Filling Station Mbezi kwa Yusuph, Camel Oil- Kibamba, Uduru Oil Station-Kibamba, Total Stop Over na Camel Oil Kimara Stop Over.


Mbali na hilo, vituo vya huduma za afya vitakavyoguswa ni Hospitali ya Boch na Kituo cha Afya cha Kimara vitakavyobomolewa nusu, Hospitali ya Neema iliyopo Kimara Stop Over, Kimara Centre Dispensary na Zahanati ya Arafa.


Wakizungumzia bomoabomoa hiyo, baadhi ya masheikh na wachungaji walisema wamepokea maagizo ya Serikali ya kutakiwa kuvunja majengo yao huku wengine, wakimuomba Rais John Magufuli kuwatazama kwa jicho la huruma.


Imamu wa Msikiti wa Jamsjid Jaria wa Kiluvya, Haidary Masenga alisema waumini wameathirika kisaikolojia kwa kutojua msikiti huo utakakohamishiwa kwa kuwa hakuna eneo walilopata.


“Ni kweli maendeleo yanahitajika na sisi hatupingi, lakini tunaomba tutazamwe kwa jicho la huruma tuachwe tuendelee kuabudu hapa. Mpaka sasa hatujui chochote tunasubiri tu hatima ya Serikali kama watavunja au la,” alisema.


Imamu Msaidizi wa Msikiti wa Kilumbi Islamic Center, Halfan Malima alimuomba Rais Magufuli kuwahurumia kwa kuwapa eneo jingine la ibada kwa kuwa bado hawajapata.


Kwa upande wake, Mchungaji wa KKKT Kibamba, Mshiu Wilness alisema kanisa limepokea agizo la kutakiwa kuhama na kubomoa jengo hilo na kwamba, tayari wameshapata eneo jingine ambalo wanatarajia kuhamia. Alisema leo kutakuwa na ibada ya mwisho kwa ajili ya kuondoka kwenye eneo hilo.


“Tumepokea, tunatarajia kuondoka na tutavunja kama tulivyoelekezwa,” alisisitiza kiongozi huyo.


Mchungaji wa Kanisa la The River Healing Ministry of Tanzania, John Kyashama alisema anaunga mkono agizo la Serikali la kubomoa nyumba, makanisa, misikiti ili kupisha upanuzi wa barabara.


Kyashama alisema hana kinyongo na Rais na anaunga mkono mipango ya maendeleo anayoifanya na anawashauri wachungaji wenzake waliokumbwa na bomoabomoa kukubaliana na hali hiyo kwa kuwa kinachofanywa na Serikali ni kwa nia njema na wananchi wake. “Si vizuri kuwa na kinyongo wala kugombana na utawala, kila mtu atii mamlaka za nchi,” alisema.


Mbali na nyumba hizo, pia Kituo Kikuu cha Polisi Mbezi Luis kitabomolewa huku Kamanda wa Polisi Kinondoni, Muliro Jumanne akisema kilijengwa kwa nguvu ya wananchi kutokana na mahitaji ya eneo hilo wakati huo.


Alisema kutokana na kuwekwa alama X, kituo hicho kitahamishiwa eneo la Gogoni kwa kuwa licha ya kuwa barabarani bado eneo lake ni dogo.


“Kituo hiki kitaondolewa hapa na kupelekwa kwenye kituo kingine cha Gogoni kilichojengwa chini ya mradi wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN),” alisema.


Alisema kituo hicho kipya pia kimeshirikisha nguvu za wananchi na ndicho kikubwa kwa Wilaya ya Ubungo.

Post a Comment

0 Comments