DAR ES SALAAM: Dunia haina huruma! Mwanaume mmoja ambaye ni mjumbe wa nyumba kumi katika Mtaa wa Kiyombo, Kinyantira-Kitunda, jijini Dar, Joshua Moniko Maranya, ambaye ni Mjumbe wa Serikali ya Mtaa, ameuawa wakati akiamulia ugomvi wa wanandoa, Risasi linakuwa la kwanza kuripoti.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Jumapili iliyopita, kiongozi mwingine wa serikali ya mtaa, ambaye alikuwa pamoja na marehemu eneo la tukio, Julita Lucas Mwanjela, alisema Jumamosi iliyopita akiwa nyumbani kwake, mkazi mmoja wa mtaani kwake ajulikanaye kwa jina la Mangi alimfuata na kumuomba afike nyumbani kwake kwani kuna ugomvi wa watu aliowakaribisha.
Wakati akielekea nyumbani kwa jamaa huyo, njiani alikutana na mjumbe mwenzake na kumuomba waungane pamoja ili kwenda kutatua mgogoro huo.
Walipofika nyumbani kwa Mangi, waliwakuta wanandoa hao wakiwa wametulia na ndipo wao walipowauliza tatizo, lakini wakasema wako sawa, na kuwataka viongozi hao kuwauliza watu waliowaambia kama wao wana ugomvi kwani hawana tatizo.
Iligundulika kuwa Mangi alimkaribisha nyumbani kwake Tumsifu na mke wake ambaye alikuwa ana mtoto mchanga.
“Kitendo cha sisi kumuuliza maswali huyo Tumsifu na baadaye kumpigia simu mwenye nyumba ambaye alisema anamtambua Mangi tu, kilimpandisha hasira Tumsifu ambaye hapohapo alianza kufanya fujo, ikiwa ni pamoja na kumpiga mwenyeji wake Mangi.
“Kuona hivyo tukatoka nje ya ua wao, tukawa tumesimama tunajadiliana tufanyeje, ndipo muuaji alitoka na kuja kumvamia mjumbe mwenzangu Moniko kwa kumpiga ngumi na mateke na kuanguka chini.
“Akiwa chini, yule jamaa alienda kuchukua mbao na kuja kumpiga nayo kwenye taya, akawa anakoroma kama mara nne hivi huku damu zikimtoka mdomoni na puani kisha akatulia, nilivyoona mwenzangu haamki, ikabidi niwaite walinzi shirikishi na kuja kumdhibiti, maana alimjeruhi pia baba mdogo wa marehemu.
“Ulinzi shirikishi wakamfungia ndani na kumpeleka kituo cha polisi huku mjumbe mwenzangu akichukuliwa kupelekwa Hospitali ya Amana ambako baada ya kupimwa alionekana ameshafariki muda mrefu,” alisema Jelita.
Akisimulia kwa huzuni kuhusu kifo cha mumewe, mke wa marehemu Sifa Kigava ambaye walibahatika kupata watoto watatu, alisema mwenzake alimuaga kwenda katika shughuli zake za kila siku za kuuza supu.
Wakati akiendelea na shughuli zake, saa tatu usiku alipata taarifa za mumewe kuwa katika hali mbaya, akidaiwa kupigwa vibaya, ambapo alikimbilia eneo la tukio lakini akakuta tayari ameshaondolewa na yeye kulazimika kurudi nyumbani baada ya kuambiwa kuwa shemeji yake na wenzake walimpeleka hospitalini.
“Kwa kweli naumia sana hata sijui nitawalea vipi hawa watoto ambao bado ni wadogo jamani, hata kuzungumza sana siwezi maana sikutarajia kwa kweli, imetokea ghafla mno,”alisema Sifa.
Naye kaka wa marehemu aliyekuwa wa kwanza kufika eneo la tukio, Yohana Maranya alisema baada ya kufika alimkuta mdogo wake akiwa amelala kifudifudi huku akiwa hajitambui, ndipo kwa kushirikiana na rafiki yake walimchukua na kumpeleka hospitali na kugundulika kuwa ameshafariki.
Baada ya tukio hilo mtuhumiwa alipelekwa katika kituo cha Polisi Staki Shari akiwa na mwenyeji wake pamoja na mwanamke aliyekuwa akigombana naye.
0 Comments