Magufuli, Museveni waweka historia

Magufuli, Museveni waweka historia



Rais John Magufuli akiwa mgeni wake Rais wa Uganda,Yoweri Museveni wakiweka jiwe la msingi la mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Tanga katika hafla iliyofanyika katika kijiji cha Chongoleani Tanga jana. Picha Ikulu

Mkoa wa Tanga jana ‘ulitekwa’ na wakuu wa nchi za Tanzania na Uganda wakati wa tukio la kihistoria la uwekaji jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.


Wakuu hao, Rais John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda walisema mradi huo utakaogharimu Sh8 trilioni utakuwa wa kihistoria na utaleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi kwa Serikali za Jumuiya ya Afrika Mashariki na wananchi wake kupitia ajira na biashara.


Viongozi hao waliokubaliana katika maeneo kadhaa wakati wa usafirishaji wa mafuta hayo kuuza katika soko la Afrika Mashariki, walitoa kauli hiyo wakati wa sherehe zilizofanyika katika Kijiji cha Chongoleani nje kidogo ya jiji hilo.


Sherehe hizo zilihudhuriwa na baadhi ya viongozi kutoka nchi zote mbili, wataalamu, wawakilishi wa kampuni za ujenzi wa mradi huo, mawaziri, wabunge, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa huku wasanii wakitoa burudani za uhamasishaji na uzalendo kwa maelfu ya wananchi waliokuwepo eneo la tukio na waliofuatilia katika vyombo vya habari.


Mradi huo utaanza Januari, 2018 huku Tanzania ikitarajiwa kunufaika na wastani wa asilimia 80 ya ujenzi huo utakaokuwa na urefu wa kilomita 1,445. Hapa nchini bomba hilo litapita katika vijiji 184, wilaya 24 na mikoa minane.


Kwa upande wa Tanzania, mradi huo utatumia Dola 3 bilioni za Marekani kati ya jumla ya Dola3.5 bilioni zitakazotumika.


Rais Magufuli aliyeonekana kuwa mwenye furaha alisema mradi huo wa kusafirisha mafuta hayo ghafi unafanyika hapa nchini ukiwa ni mkubwa kuliko yote iliyowahi kujengwa duniani kote.


“Hili bomba ni la aina yake, tuna bomba la Songosongo hadi Dar es Salaam lenye kilomita 232, pia tuna bomba la kutoka Mnazi Bay hadi Dar es Salaam lenye kilomita 522, pia tuna bomba la kutoka Kigamboni hadi Zambia (Tazama) lenye urefu wa kilomita 1,710,” alisema.


“Sasa hili lina tofauti na mabomba mengine yote, nafikiri duniani hakutakuwa na bomba lenye urefu huu wa kusafirisha mafuta yaliyochemshwa, bomba refu kwa taarifa nilizo nazo liko India lenye kilomita 600, kwa hili la kilometa 1,445 litakuwa la kwanza duniani,” alisema.


Pili, Rais Magufuli alisema litasaidia kuzalisha ajira 1,000 wakati wa uzalishaji, ajira 30,000 za vibarua wakati wa ujenzi wa mradi na shughuli za biashara zitaongezeka.


“Na fursa zimeshaanza kuonekana, wenye gesti (nyumba za kulala wageni) leo zimejaa Tanga, hata Muheza, Korogwe,” alisema.


Tatu, baada ya mradi huo kukamilika, utasaidia kuchochea ujenzi wa kiwanda cha saruji ambacho kitazalisha tani bilioni mbili kwa mwaka.


Rais alisema kiwanda hicho kitakuwa kikubwa kuliko vyote nchini.


Nne, alisema baada ya mradi huo, bomba litakuwa likitoa mapipa 216,000 huku Serikali ya Tanzania ikinufaika na mapato ya Dola12.5 kwa kila pipa huku akiahidi mapipa hayo kuongezeka wakati wa uzalishaji.


Tano, Rais Magufuli alisema mradi huo ukikamilika utachochea ujenzi wa viwanda vidogo vya mafuta mkoani Tanga ambavyo vitasaidia kushuka kwa gharama za manunuzi yanayofanyika kwa sasa nje ya nchi.


“Sisi tunanunua ‘crude oil’ (mafuta ghafi) kwa sasa kutoka Uarabuni, hakutakuwa na sababu ya kwenda kununua tena huko wakati kuna crude oil itakayopatikana Tanga, naamini watatuuzia kwa bei nzuri, hiyo nayo ni fursa kubwa kwetu,” alisema.


Faida ya sita, Rais Magufuli alisema kupitia mradi huo Serikali za nchi hizo zimeshaanza mazungumzo ya kutumia watalaamu wake ili wafanye kazi ya kutafuta mafuta yaliyopo katika Ziwa Tanganyika na Eyasi. “Na Rais (wa Uganda) ameshakubali watalaamu hao wakacheki mafuta hayo tukishayachimba huko tunayaunganisha katika bomba hili, na hayo ndiyo maendeleo tunayoyataka kwa nchi za Afrika Mashariki,” alisema.


Pia, Rais alisema licha ya kuzalishwa kwa mafuta ya taa, petroli, dizeli na ya ndege, bidhaa nyingine zitatokana na malighafi ya plastiki.


Mbali na hatua hiyo, Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake na Rais Museveni walikubaliana gesi inayotoka Mtwara iweze kusafirishwa kwenda Uganda.


“Angependa (Museveni) litengenezwe bomba lingine mbadala liende hadi Uganda ili na sisi tukauze gesi yetu kule, wao wanaleta huku (mafuta) na sisi tunapeleka kule,” alisema.


Kuhusu ulinzi, alimuhakikishia Rais Museveni kuwapo kwa ulinzi wa kutosha huku akimwomba kushirikiana katika uwezeshaji wa posho za kujikimu kwa askari 1,115 watakaohusika katika kazi hiyo.


“Hili bomba kwa upande wa Tanzania lina kilomita 1,115, ukigawa kwa kilomita moja moja tunakuwa na askari 1,115, kwa hiyo ulinzi ni imara,” alisema.


Rais Magufuli aliwaomba wakandarasi kuharakisha mradi huo kabla ya mwaka 2020 kwa kutumia wakandarasi na rasilimali zilizopo.




Aonya na kutoa ahadi


Rais Magufuli alitoa onyo kali kwa wakazi wa Tanga na maeneo ambapo bomba hilo litapita kwa lengo la kupata fidia akisema, “wameula wa chuya.”


Alisema tayari zipo picha za eneo lote na wahusika watakaolipwa huku akitahadharisha walio katika maeneo yasiyostahili kisheria.


Katika hatua nyingine Rais Magufuli ambaye alifika kwa mara kwanza Tanga wiki hii tangu alipoingia madarakani, alitumia nafasi hiyo kutoa ahadi yake kwa wananchi.


Alisema Serikali yake itaanza ujenzi wa barabara ya lami kutoka Tanga hadi Bagamoyo yenye urefu wa kilometa 175 na upembuzi yakinifu umeshakamilika huku fedha zikitoka Benki ya Maendeleo ya Afrika.


Vilevile, aliahidi kufufua viwanda kadhaa katika mkoa huo na baadhi yake leo ataanza kuviwekea mawe ya msingi.


Alisema anataka kuirudishia Tanga hadhi ya viwanda vilivyokuwapo miaka ya nyuma.


Pia, aliahidi kurejesha ardhi iliyokuwa imepokonywa kwa wanyonge ambao ni wakulima, jambo lililowafanya kukosa maeneo ya kilimo. “Nimetoa maagizo katika mashamba 72 yameshapitiwa, mashamba 12 yameandikiwa notisi ya siku 90 wakishindwa wanyang’anywe na mashamba matano yenye hekta 14,000 nimeshayafuta na yatarudishwa kwa wananchi wagawiwe bure ili walime, wasipolima watanyang’anywa na wao,” alisema.




Museveni atoa ya moyoni


Kabla ya Rais Magufuli kuzungumza, Rais Museveni aliweka wazi uhusiano wake na Tanzania akisimulia jinsi alivyopitisha bunduki 14 za magendo kutoka mji wa Horohoro na baadaye Mkoa wa Tanga enzi za kuwania kuingia madarakani nchini Uganda.


Alisema bunduki hizo alizitumia kufanikisha mpango huo.


Kabla ya kueleza tukio hilo, kiongozi huyo alianza kutafsiri uhusiano wa Uganda na Tanzania akisema ni makosa kufananisha ndugu na rafiki akimaanisha Tanzania ni ndugu wa Uganda.


Pia, alieleza jinsi gani nchi za Afrika Mashariki zinaweza kujikomboa na umaskini bila kutegemea misaada kutoka nje na kutoa mfano wa rasilimali zilizopo, ukubwa wa soko na nguvukazi iliyopo.


Alisema kwa sasa ukinunua gari kutoka China, Japan au nchi nyingine kutoka mataifa tajiri ni kuyatajirisha na kunufaisha watoto wao, hivyo ni wakati wa kujipanga ili rasilimali za Afrika Mashariki ziwanufaishe watoto waliopo.


Rais Museveni ambaye ni mwenyeji hapa nchini, alisema Uganda ina mpango wa kufufua kampuni ya ndege na uzalishaji wa mafuta utakaoanza utasaidia kuinua uchumi kwa Taifa hilo na Afrika Mashariki kwa ujumla.


Alisema kwa kuwa Tanzania itazalisha gesi kutoka mkoani Mtwara, baada ya kukamilika kwa mradi huo wa bomba la mafuta ameomba ianze kupelekwa nchini Uganda ambako kuna uhitaji mkubwa wa nishati hiyo pamoja na makaa ya mawe.


“Tunataka bomba ingine (jingine) ije (lije) kule (Uganda), bomba mbili zikutane njiani, ” alisema.


Rais Museveni alisema waliichagua Tanzania kupitisha mradi huo wa bomba kwa sababu ya kuwaondolea mambo kadhaa yenye faida kwao. “Tanzania imetupa faida pia, imetuondolea kodi ya usafirishaji, kodi ya VAT na kodi ya mapato, asante sana, na ndio maana mradi huu utakuwa na faida,” alisema.


Kiongozi huyo alisema shughuli zitakazoambatana na uzalishaji wa mafuta zitachochea uharakishaji wa miradi mbalimbali ikiwamo ujenzi wa reli, barabara na kilimo cha umwagiliaji.




Maandalizi ya mkoa


Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martine Shigella alitumia nafasi hiyo kumuomba Rais Magufuli kufufua ujenzi wa Bandari ya Tanga, ombi ambalo alilipokea.


Shigella alisema uongozi wa mkoa huo tayari umeshaanza kuandaa mazingira ya kusaidia upatikanaji wa maeneo ya ardhi kwa ajili ya ujenzi wa makazi ya wawekezaji wakati wa utekelezaji wa mradi huo.


Shigella alisema mbali na hatua hiyo, pia wanawahakikishia wawekezaji na Watanzania kupata maeneo ya ofisi zitakazohusika kwenye utekelezaji wa mradi huo.


“Tumeshaanza kuhimiza watoto wetu waende vyuoni ili wapate ujuzi utakaowasaidia kuajiriwa wakati wa mradi, fursa zilizopo zitasaidia kuinua kipato cha wakazi na kupunguza umaskini, kwa hiyo mheshimiwa Rais wakazi wa Tanga wanaomba useme neno moja tu na roho yao itapona,”alisema.




Mawaziri wa madini


Naibu Waziri wa Nishati na Madini nchini, Dk Merdadi Kalemani alisema mradi huo utawanufaisha wakazi wa vijiji 184, wilaya 24 na mikoa minane nchini.


Alisema vijiji hivyo vinapatikana katika wilaya 24 kwenye mikoa ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga.


Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Irene Muloni alisema mradi huo utachochea shughuli za kibiashara kupitia utoaji huduma na manunuzi ya bidhaa.


Pia, Muloni aliishukuru Tanzania kushirikiana na Uganda kwa ajili ya mradi alioutaja kuwa utakuwa mkubwa na wa aina yake.




Alisema kupitia uzoefu wa Tanzania katika ujenzi wa mabomba ya gesi na mafuta pamoja na wataalamu waliobobea, anaamini utakwenda kwa kasi na kukamilika kwa wakati.


















Post a Comment

0 Comments