Mstaafu adai bomoabomoa ‘imemwambukiza’ ugonjwa

Mstaafu adai bomoabomoa ‘imemwambukiza’ ugonjwa


Mkazi wa Kimara Suka, John Mlangi akiwa amesimama mbele ya nyumba juzi aliyokuwa akifanyia biashara kabla yaigeuza nyumba ya Ibada. Nyumba hii pamoja na ayoishi (kulia) zimwekwa alama ya x kwa ajili ya kuvunjwa ili kupisha upanuzi wa Barabara Morogoro. Picha na Salim Shao 

Mkazi wa Kimara Stop Over, John Mlangi (74), amesema hataondoka katika nyumba yake iliyowekwa alama ya ‘X’ kwa ajili ya kubomolewa na ameapa kuwa yupo tayari kuzikwa ndani ya jengo lake iwapo litabomolewa.


“Nyumba yangu ndio kaburi langu, ikiwa kweli watabomoa basi nami watanizika hapahapa kwa sababu sina tena nguvu ya kufanya kazi, naumwa sana tangu waniwekee ‘X’, nimepata presha ugonjwa mpya wa shikikizo la damu,” amesema mzee huyo katika mahojiano na Mwananchi.


Haikuwa rahisi kusikiliza simulizi ya mzee huyo ambaye nyumba yake na jengo alilogawa kwa ajili ya kanisa kuwa miongoni mwa yatakayokumbwa na bomoabomoa hiyo.


Nyumba hiyo na nyingine zinatakiwa kubomolewa ili kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) kuziwekea alama ya X nyumba kadhaa kuanzia Kimara mpaka Kiluvya.


Katika mahojiano hayo na Mwananchi, kuna wakati mzee huyo aliinama chini na wakati mwingine kufuta machozi kutokana na huzuni aliyonayo.


Mzee Mlangi alisema ilibidi asafirishwe kwenda nje ya nchi kwa ajili ya matibabu, lakini imeshindikana kwa sababu ya bomoabomoa hiyo.


Alisema kwamba, licha ya presha pia anaumwa nyonga na miguu na kwamba hana uwezo wa kutembea peke yake bila msaada wa magongo mawili.


“Matibabu ya maradhi yangu yameshindikana hapa nchini nikashauriwa niende nje, wakati tukiwa katika kuhangaikia suala hili wakaja kutuwekea X hapa nyumbani. Kwa hiyo sijui nifanye nini tena,” alisema.


Mzee huyo alisema alijenga nyumba yake miaka 35 iliyopita na wakati huo hakukuwa na sheria yoyote ya ardhi aliyokuwa ameivunja kwa kuwa alikuwa nje ya mita 60 kutoka kwenye barabara.


Aliongeza kuwa kiwanja cha nyumba yake kilinunuliwa kihalali na kwa miaka hiyo yote alikuwa akilipa kodi ya majengo kwa sababu hakuvunja sheria.




Maisha yake


Mzee Mlangi aliijenga nyumba yake kutokana na kazi ya uhandisi aliyokuwa akiifanya kabla hajastaafu.


Alisema aliwahi kuongoza taasisi mbalimbali ikiwamo kuwa meneja wa Tanzania Planting Company (TPC) mwaka 1992 na kazi hizo ndizo zilizomwezesha kujenga nyumba hiyo.


Alisema baada ya kustaafu aliamua kuwekeza kwenye kilimo cha miwa wilayani Kilombero, lakini tangu alipougua ameshindwa kuendeleza shughuli za kumuingizia kipato.


Mbali na kilimo, mzee huyo alisema aliamua kufungua kampuni ya ushauri kuhusiana na masuala ya uhandisi ambayo aliifunga kutokana na hali yake kiafya.


“Vijana wote niliokuwa nimewaajiri ilibidi waende wakatafute kazi nyingine kwa sababu nimeshazeeka na sina uwezo tena wa kufanya kazi kama zamani,” aliongeza.


Alisema aliamua kuwekeza kwenye biashara ya vinywaji kwa kujenga eneo la biashara zake ambalo pia alilazimika kuligawa kwa ajili ya kanisa kutokana na kushindwa kuliendesha.


Hata hivyo alisema kilichobaki kwake kwa sasa ni maumivu na tangu awekewe ‘X’ amekuwa akiishi kwa hofu.


“Nipo kwenye matibabu ya presha, inanisumbua sana kwa kweli kwa sababu naishi kwa hofu kupita kiasi,” alisema.


Kuhusu matibabu yake nje ya nchi, Mlangi alisema hajajua kama anaweza tena kwenda kutibiwa mpaka hatma ya nyumba yake itakapokamilika.


Mwenyekiti wa Mtaa wa Stop Over, Magreth Msabuso alisema wapo wazee wengi waliostaafu ambao ikiwa nyumba zao zitabomolewa bila fidia hali zao zitakuwa mbaya.


Alisema wananchi walipaswa kushirikishwa tangu hatua ya kwanza wakati wanataka kuweka alama ya ‘X’.


















Post a Comment

0 Comments