Wakazi wa Kata ya Mngazi, Wilaya ya Morogoro wamesema migogoro ya ardhi iliyokuwa imekithiri katika maeneo yao imepungua kutokana na ushirikiano wao, ambapo awali shughuli za maendeleo ndani ya jamii zilikwama.
Wananchi hao wamesema hayo wakati wakizungumza na mwandishi wa Mwananchi aliyekuwa katika kata hiyo kwa nia ya kufahamu namna migogoro ya ardhi inavyotatuliwa maeneo ya vijijini.
“Migogoro ya ardhi imepungua kutokana na wananchi kutambua njia sahihi ya kutatua migogoro na namna ya kuepuka isitokee tena katika maeneo yetu kwani watu wengi wameuawa na wengine kujeruhiwa,” amesema Asha Ally.
Amesema migogoro ya ardhi iliyokuwa inasumbua katika eneo lao ni pamoja na mipaka, mashamba ya urithi na baadhi ya viongozi wa vijiji kuuza maeneo bila ya kuwashirikisha wananchi, lakini hivi sasa haipo tena kutokana na wengi kupata uelewa, kujua nia sahihi ya kutatua na madhara ya migogoro ya ardhi.
Amesema kwa sasa wananchi wengi wamebadilika baada ya kupata elimu ya umiliki wa ardhi kutoka Kituo cha Wasaidizi wa Kisheria (MPLC) kupitia mradi wa kulinda haki za mwanamke katika kumiliki ardhi unaofadhiliwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Foundation for Civil Society.
Mkazi mwingine, Athuman Seif amesema mradi huo umesadia jamii yao kupatiwa hatimiliki za kimila za ardhi wanayotumia, hivyo kila mmoja kujua mipaka ya eneo lake baada ya kupimiwa na kuepuka muingiliano ambao unaweza kuzua mgogoro.
“Maeneo mengi ya kwetu migogoro ya ardhi ilikuwa inatufanya tushindwe kufanya shughuli nyingine za maendeleo, hivi sasa muda mwingi tuko shambani kulima na sio kushinda baraza la ardhi kusikiliza kesi kama hapo awali,”amesema Seif.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Vigolegole, Octavian Kobelo amesema hivi sasa kesi za ardhi katika baraza la ardhi kata zimepungua na kuwa, kabla ya mradi huo walikuwa wanapokea kesi 10 kwa mwezi, lakini kwa sasa kesi moja inapokelewa na kufanyiwa kazi.
0 Comments