Mwigulu atoa Sh15 milioni ujenzi wa kanisa kutokana na bomoabomoa

Mwigulu atoa Sh15 milioni ujenzi wa kanisa kutokana na bomoabomoa



Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba (kushoto) akizungumza jambo na Askofu wa Kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa baada ya misa ya harabee kwa ajili ya mchango wa ujenzi wa kanisa la Mbezi Luis jijini Dar es Salaam jana. Katikati ni Mchungaji wa kanisa hilo, Oscar Mlyuka. Picha na Ericky Boniphace 

Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba amechangia Sh15 milioni katika harambee ya ujenzi wa kanisa jipya la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Luisi baada ya kanisa la awali kukumbwa na bomoabomoa ya kupisha upanuzi wa barabara ya Morogoro.


Kanisa hilo ni moja kati ya nyumba zaidi ya 30 za ibada zilizowekewa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) ili kupisha upanuzi wa barabara hiyo kuanzia Kimara hadi Kiluvya.


Katika harambee hiyo, Mwigulu pia alipiga mnada picha yake na kuiuza kwa Sh 3 milioni kwa ajili ya ujenzi huo.


Akizungumza katika ibada hiyo maalumu iliyoendeshwa na Askofu wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa, Mwigulu aliwapongeza waumini kwa hatua waliyofikia ya kujenga kanisa kubwa na kuwasihi kuendelea kumuombea Rais John Magufuli na Taifa.


“Kwanza niwapongeze kwa hatua hii mliyofikia ya ujenzi wa kanisa kubwa tena la kisasa, lakini naomba niongee vitu viwili, cha kwanza naomba tuendelee kuliombea Taifa kwani mambo yamebadilika, baadhi ya wananchi wanzetu wamekosa uzalendo na nchi yao wanashiriki kufanya uhalifu,” alisema.


Alisema kuna taarifa ambazo wanazipata za baadhi ya Watanzania kushiriki kufanya mambo mabaya jambo ambalo hajawahi kufikiria kama ipo siku watafikia hatua hiyo, lakini ukweli ni kwamba wapo na wengi ni watoto ambao wanakwenda nje ya nchi kujifunza ugaidi.


“Mfano mzuri ni wilaya yetu ya Kibiti, tumebaini watoto wetu wanafanya mambo haya ukielezwa unaweza usielewe lakini ukifika na kuona utajua kuwa ni mambo ya ajabu yanayofanywa na baadhi ya Watanzania wenzetu,” alisema.


Mwigulu pia aliwaasa waumini hao kuendelea kumuombea Rais kwani hatua anazochukua ni kwa makusudi mazuri ya kuleta maendeleo na kwamba yupo katika vita kali ambayo kwa nguvu ya kibinadamu tu hataweza.


“Ukiona Rais anafanya maamuzi, jua kuna mambo mazuri anataka yafanyike, mkiona anabana matumizi, mjue kabisa kuna mambo mazuri yanakuja na hayo mambo mazuri ni kwa ajili ya manufaa yetu hata Rais akiondoka madarakani hawezi kuondoka nayo,” alisema.


Alisema kuna watu wanamuona Rais ni mkali na kusisitiza kuwa mtu anayepambana na ufisadi kamwe hawezi kuwa mpole, “Lazima awe mkali hata Yesu alipokuwa anakemea mapepo alikemea kwa ukali, ndivyo hata Rais anavyofanya pale anapopambana na uovu wa nchi.”


Pia Mwigulu aliwasihi waumini kujitoa kwa hali na mali katika kuchangia fedha kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa kanisa hilo kwani kuna siri kubwa kwa mtu anayechangia ujenzi wa nyumba za ibada huku akiwaomba waumini kuendelea kujenga makanisa mengi.


“Nimegundua ndani ya nyumba za ibada kuna siri kubwa, utafiti niliofanya mdogo nimekuja kukundua mikoa ambayo ina nyumba nyingi za ibada hawana matatizo mengi kama vile mabaa ya njaa, mfano mzuri ni mikoa ya Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Ruvuma na Njombe, kila mtaa kuna kanisa,” alisema.


Alisema mikoa ambayo haina nyumba nyingi za ibada ni Kagera, Dodoma, Tabora na Shinyanga. “Huko kupata kanisa ni kwa shida angalia sasa kila siku wao wanalia njaa Mbeya, Iringa chakula ni cha kumwaga,” alisema.




Askofu Malasusa


Akiendesha ibada ya harambee ya ujenzi wa kanisa hilo, Askofu Malasusa alisema jambo lolote linapotokea lina makusudi. Alisema kuambiwa kuhama ili kupisha upanuzi wa barabara ni baraka kutoka kwa Mungu hivyo hawana budi kuipokea.


“Hiyo ni baraka, unapopatwa na misukosuko usifikiri itakupeleka pabaya, Mungu yuko pamoja nanyi zaidi naomba muendelee kumwabudu Mungu, kumpenda na kuwa na amani. Mshukuruni Mungu maana amewapa akili ya kujenga kanisa lingine kubwa.”


Alisema wapo wachungaji wengine ambao ni maarufu lakini bado hawajapata baraka ya kujenga makanisa makubwa kama wao.


Katika harambee hiyo, waumini hao walichangia vitu mbalimbali baadhi walitoa mali zao na kuzipiga mnada wakiongozwa na askofu huyo ambaye alipiga mnada picha yake na kuiza kwa Sh3.5 milioni.


Waumini wengine walitoa mali mbalimbali kama vitenge, mbuzi na kuku kwa ajili ya kupigwa mnada ili kupata fedha zitakazosaidia kukamilisha ujenzi wa kanisa jipya.


Post a Comment

0 Comments