Staili mpya ya unywaji wa ‘viroba’ yabainika

Staili mpya ya unywaji wa ‘viroba’ yabainika



Baada ya Serikali kupiga marufuku matumizi ya pombe kali zinazofungashwa kwenye mifuko ya plastiki maarufu viroba, wauzaji na watumiaji wake wameibuka na mbinu mpya ya kupata kinywaji hicho.


Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili umeshuhudia vibanda kadhaa vinavyouza bidhaa mbalimbali katika maeneo ya vituo vya madereva wa bodaboda vikiuza pombe kali katika kipimo cha Sh500, Sh700 na Sh1,000 ambayo huwekwa kwenye vikombe vidogo.


Biashara hiyo imeonekana kushamiri katika vituo vya Tabata Shule, Tabata - Mwananchi, Kinondoni Studio, Mkwajuni na Buguruni Sheli.


Machi mosi mwaka huu, Serikali ilitangaza kusitishwa kwa biashara ya viroba kutokana na athari zake kwa jamii hasa kwa vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya Taifa.


Hatua hiyo ilikuwa ni utekelezaji wa agizo lililotolewa Februari 18 na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipohutubia wakazi wa Mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kabla ya kutiliwa mkazo na Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira), Januari Makamba.


Viroba hivyo vilikuwa vikizalishwa na kampuni za vinywaji na kuuzwa kwa bei ya kati ya Sh700 hadi Sh1,500 na wateja wakubwa walikuwa ni watu wa hali ya chini wakiwamo bodaboda.


Kutokana na zuio la Serikali lililodumu kwa miezi mitano sasa, wafanyabiashara wamegundua mbinu hiyo mpya ya kuuza viroba kwa kupima ili kulinda soko la wateja wao.


Madereva wa bodaboda waliozungumza na gazeti hili walikiri kukithiri kwa biashara hiyo huku baadhi yao wakipongeza na wengine wakikemea kwa kuwa inaathiri utendaji wa kazi kwa madereva wengi.


“Vipimo vinakuwa vikombe vidogo, vinafanana na vikombe vya kahawa, lakini vinatofautiana ujazo, mimi hununua vikombe viwili hadi vitatu vya Sh700 kwa siku, natumia jioni tu baada ya kumaliza kazi,” alisema Charles Temba.


Khamis Mayunga anayefanyia shughuli zake Kinondoni Studio alisema biashara hiyo imekuwa ya kawaida na ni sehemu ya chanzo cha ajali za bodaboda.


“Mie natumia kilevi hicho na huwa naweza kununua asubuhi kipimo cha Sh500, mchana na jioni kulingana na mahitaji yangu niliyokuwa nikitumia kabla ya kufungiwa viroba,” alisema.


Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Awadhi Haji alisema polisi haijawahi kuwakamata madereva bodaboda waliotumia kilevi na hawana takwimu hizo.


















Post a Comment

0 Comments