Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula ameziagiza halmashauri zote kuwafikisha mahakamani na kuuza mali zao wadaiwa wote sugu wa kodi ya ardhi ambao wana madeni ya muda mrefu.
Mhe. Mabula ametoa agizo hilo wakati alipofanya ziara ya kukagua mifumo ya makusanyo ya kodi ya ardhi mkoani Geita mara baada ya kukuta majina 100 ya wadaiwa sugu wa kodi ya ardhi ambao hawajalipa kodi kwa zaidi ya miaka 10.
Mhe. Naibu Waziri wa Ardhi alimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita kuhakikisha wadaiwa hao wa muda mrefu wanaandikiwa notisi ya muda wa siku 14 na wasipolipa ndani ya muda huo wafikishwe mahakamani bila kuchelewa na kama wasipolipa basi mali zao zipigwe mnada.
Aidha, Naibu Waziri huyo alitembelea eneo lenye viwanja vilivyowekwa mpango wa matumizi bora ya ardhi katika wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita ambavyo vimepangwa kujengwa ofisi za serikali, shule, hospitali, makazi, maeneo ya kuzikia, na huduma nyingine za kijamii.
Naibu Waziri alimtaka mkuu wa wilaya ya Nyang’hwale kuhakikisha mji huo unapangwa vizuri na kuwekwa miundombinu ya barabara, maji safi na taka na umeme ili kuepusha migogoro ya ardhi ambayo mara nyingi huibuka kutokana na wilaya kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi ya muda mrefu.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angeline Mabulla anaendelea na ziara yake ya mikoa ya kanda ya ziwa ambapo anataria kufanya ziara Mkoa wa Shinyanga hasa katika wilaya za Kahama na Shinyanga Mjini.
0 Comments