Azam FC yaishushia kipigo kizito Friends Rangers

Azam FC yaishushia kipigo kizito Friends Rangers


Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, hapo jana usiku imeishushia kipigo cha mabao 6-0 timu ya Friends Rangers katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam complex, Chamazi, Dar es Salaam.


Mchezo huo ulikuwa ni maalum kwa jili ya maandalizi kuelekea mtanange ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Lipuli utakaofanyika ndani ya dimba hilo Jumapili hii Septemba 24 mwaka huu.

Azam FC ilitakata vilivyo katika kila kipindi, ambapo ilijipatia mabao mawili ya uongozi kipindi cha kwanza kupitia kwa nahodha wake, Himid Mao ‘Ninja’, aliyefunga la kwanza dakika ya 18 akimalizia pasi safi ya Yahya Zayd.

Mao alitupia jingine dakika 10 baadaye kwa njia ya mkwaju wa penati kufuatia mshambuliaji Mbaraka Yusuph, kuangushwa ndani ya eneo la hatari wakati akienda kumtungua kipa wa Friends Rangers.


Kipindi cha pili Kocha Mkuu wa Azam FC, Aristica Cioaba, alikibadilisha kikosi chote kilichoanza isipokuwa beki David Mwantika, aliyebakishwa na kuwa nahodha wa kikosi hicho kabla ya kupumzika dakika ya 79 na kuingia kiungo Salmin Hoza.

Katika kipindi hicho, Azam FC ilijiongezea mabao mengine manne na kuhitimisha ushindi huo, ambapo mshambuliaji Wazir Junior alihusika kwenye mabao mawili akifunga dakika ya 65 na 65.

Winga anayekuja kwa kasi Idd Kipagwile, aliipatia Azam FC bao la tano dakika ya 86 baada ya kuipokea pasi safi ya juu iliyopigwa na Hoza kabla ya kumpiga chenga kipa na kufunga bao hilo.

Ushindi huo ulihitimishwa kwa bao maridadi la Joseph Mahundi dakika ya 89, aliyeipokea pasi safi ya Hoza na kupiga shuti la umbali lililotinga wavuni.

Kikosi cha Azam FC mara baada ya mchezo huo kitaendelea tena na mazoezi hii leo jioni siku ya Alhamisi kwaajili ya maandalizi ya kuivaa Lipuli ya Iringa Jumapili ya wikiendi hii.

Kikosi cha Azam FC hapo jana:

Razak Abalora /Mwadini Ally dk 46, Daniel Amoah/Swalehe Abdallah dk 46, Bruce Kangwa/Hamim Karim dk 46, Agrey Moris/Abdallah Kheri dk 46, David Mwantika/Salmin Hoza dk 79, Himid Mao (C)/Masoud Abdallah dk 46, Stephan Kingue/Braison Raphael dk 46, Frank Domayo/Joseph Mahundi dk 46, Yahya Zayd/Wazir Junior dk 46, Mbaraka Yusuph/Idd Kipagwile dk 46, Enock Atta/Ramadhan Singano dk 46

Post a Comment

0 Comments