Diego Costa awasili Atletico Madrid kukamilisha Usajili

Diego Costa awasili Atletico Madrid kukamilisha Usajili



MSHAMBULIAJI Diego Costa amewasili mjini Madrid tayari kukamilisha uhamisho wake wa kurejea klabu yake ya zamani, Atletico Madrid.

Mwanasoka huyo wa kimataifa wa Hispania, amesafiri kutoka nchini kwake, Brazil ambako alikuwa ametulia baada ya kuachana na mabingwa wa Ligi Kuu England.

Atletico imeposti kwenye ukurasa wake wa Twitter picha ya Costa akiwa Uwanja wa Ndege wa Adolfo Suarez Madrid Barajas na maelezo; "Atleticos, rafiki anawasalimia!" baada ya mshambuliaji huyo kuwasili nchini Hispania.

Atletico Madrid imefikia makubaliano na Chelsea juu ya uhamisho wa mshambuliaji huyo, Costa kurejea klabu ya Hispania.

Atletico Madrid imesema kwamba Chelsea imempa ruhusa mshambuliaji huyo kusafiri kwenda Madrid siku zijazo kufanyiwa vipimo vya afya katika kukamilisha mkataba wa kurejea kwenye klabu yake.

Inafikiriwa Costa atasaini kwa dau la Pauni Milioni 53 ifikapo mwezi Januari mwaka 2018, kufuatia kutofautiana na kocha wa Chelsea, Antonio Conte ambayo imesababisha asitumiwe kwenye kikosi cha The Blues hadi sasa msimu huu.

Costa ataruhusiwa kucheza Atletico ifikapo Januari, wakati klabu hiyo itakapomaliza adhabu yake ya kufungiwa na FIFA kusajili wachezaji wapya.

Alijiunga na Chelsea kutoka Atletico Julai mwaka 2014 kwa ada ya Pauni Milioni 32 kwa mkataba wa miaka mitano.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 aliisaidia klabu hiyo kutwaa mataji mawili ya ubingwa wa Ligi Kuu ya England, akifunga mabao 59 katika mechi 120 alizocheza kwenye mashindano yote.

Lakini alijikuta anaingia kwenye matatizo na kocha wa sasa wa Chelsea, Antonio Conte, ambaye aliripotiwa kumtumia ujumbe wa maandishi kwenye simu kwamba hayumo mipango ya timu ya msimu huu.

Mara moja, Costa akamlalamikia Conte hadharani na kuzungumzia nia yake kutaka kurejea Atletico, timu ambayo alijiunga nayo kwa mara ya kwanza mwaka 2007.

Hawezi kucheza Atletico kwa sasa kwa sababu klabu hiyo inatumikia adhabu ya kufungiwa na FIFA kusajili wachezaji wapya hadi mwaka 2018 baada ya kukiuka taratibu za usajili kwa kumsajili mchezaji aliye chini ya umri. Kwa sasa, klabu hiyo inasajili wachezaji wapya, lakini hawawezi kucheza hadi klabu imalize adhabu.

Costa hajacheza Chelsea tangu wafungwe kwenye fainali ya Kombe la FA England na Arsenal mwezi Mei mwaka huu.

Ikumbukwe, Atletico watakuwa wenyeji wa Chelsea katika mchezo wa Kundi C Ligi ya Mabingwa Ulaya mjini Madrid, Hispania Jumatano ya Septemba 27, mwaka huu.

Post a Comment

0 Comments