Shughuli za EALA zakwamishwa na uchaguzi wa Kenya

Shughuli za EALA zakwamishwa na uchaguzi wa Kenya


Vikao vya Bunge la Afrika Mashariki(EALA) vimeendelea kukwama kuanza kutokana na hatua ya hatua ya Kenya kushindwa kuteua wabunge wake hali ambayo imesababisha maazimio ya bunge hilo yaliyopaswa kufanyiwa kazi kushindwa kutekelezwa.

Hadi sasa nchi nyingine wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeshateua wabunge wake wanaofikia tisa lakini kushindwa kupatikana kwa wawakilishi kutoka Kenya kumefanya shughuli za bunge hilo kuendelea kusimama.

Baadhi ya shughuli zilizosimama ni pamoja kushindwa kujadiliwa na kupitishwa miswada 13 kuwa sheria, kutoteuliwa kwa Spika mpya na kukosekana kwa wakuu wa kamisheni ya bunge.

Ofisa Mkuu wa Uhusiano Mwema wa EALA, Bobi Odiko ameliambia gazeti la New Times la Rwanda kuwa, wabunge hao walitazamiwa kuapishwa Juni 6 mwaka huu na kuanza vikao vyao mara moja, lakini hilo halijafanyika hadi sasa kwa kuwa Kenya haijateua wanachama wake tisa wa kuiwakilisha katika taasisi hiyo ya kikanda.

Amesema nchi zote wanachama wa EAC zimekwishawateua wabunge wake isipokuwa Kenya na kwa msingi huo, vikao vya bunge hilo vitaendelea kuahirishwa hadi Kenya itakapoteua wanachama wake.

Maofisa wa EALA wamesema hatua ya Mahakama ya Juu ya Kenya kubatilisha matokeo ya urais huku Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Kenya (IEBC) ikisogeza mbele tarehe ya uchaguzi wa marudio umezidi kuathiri sura ya bunge hilo.

Wabunge wa Bunge la 12 la Kenya waliapishwa Agosti 31 mwaka huu na baadaye bunge hilo liliziandikia barua nchi wanachama wa EAC, likisisitiza kuwa uteuzi wa wabunge tisa wa EALA utapewa kipaumbele mara shughuli za bunge zitakapoanza.

Bunge la 11 la Kenya lilishindwa kufanya uteuzi wa wawakilishi wake baada ya kambi ya serikali na upinzani bungeni kulumbana kuhusu majina yaliyopendekezwa. Mvutano wa aina hiyo uliwahi kushuhudiwa nchini wakati kambi ya upinzani iliposhindwa kupata wawakilishi wake kwa wakati.

Bunge hilo lililazimika kurudia uchaguzi wa kuwapata wawakilishi wa Chadema baada ya wale waliojitokeza mwanzo kupigiwa kura ya hapana kwa kile kilichoeleza kutokidhi vigezo.

Post a Comment

0 Comments