Vurugu zilizoibuka wakati wa kuvunja vibanda katika bonde la Jangwani zimesababisha basi na kituo cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kuvunjwa vioo kwa mawe.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Udart, Deus Bugaywa amesema bado hawajafanya tathmini kujua thamani ya mali iliyoharibiwa.
Akizungumzia uvunjaji wa vibanda hivyo ulifanyika leo Jumatano, msemaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa), Nelly Msuya amesema umetekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili kuwapisha Dawasa kujenga mtambo wa maji taka.
“Kazi ya ujenzi wa mradi inaanza kesho ikiwamo kujenga uzio na kuandaa mazingira. Ukija hapa kesho utapata kila kitu kuhusu mradi,” amesema Msuya.
Amesema nyumba zilizokuwa eneo hili zilishavunjwa na kwamba, kilichokuwepo ni mabanda.
Wakati wa shughuli hiyo, baadhi ya wananchi waliokuwa wakiishi eneo hilo wakiungana na wengine walifanya vurugu wakipambana na askari wa jiji waliokuwa wakisimamia ubomoaji huo.
Wakazi hao, wengi wakiwa vijana walirusha mawe na chupa hivyo polisi walilazimika kuingilia kati kudhibiti vurugu hizo na kuendelea kuweka doria ili kuimarisha usalama.
Wakati ubomoaji ukifanyika, mvua ilikuwa ikinyesha hivyo mali za wananchi hao zilizokuwa zimetolewa ndani ya mabanda hayo zikiwemo magodoro, vitanda na nguo zililowa.
Wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo wameeleza kushangazwa na uamuzi wa wao kuwaondoa bila kupewa muda wakati wamekuwepo hapo kwa miaka mingi.
“Tumekaa hapa muda mrefu tukifanya shughuli za kilimo na kama mnavyoelewa utamaduni wetu, mtu unapolima unaweka na kibanda chako papo hapo sasa tunashangaa kuondolewa, wanataka twende wapi hatuna pa kwenda,” amesema Mahija Khamis.
Mkazi mwingine, Zaitun Mohamed amesema kitendo hicho ni unyanyasaji kwa kuwa hakuna fidia waliyolipwa kwa nyumba zao kubomolewa.
0 Comments