Aliyekuwa Makamu Mwenyekiti NCCR-Mageuzi (Bara), Leticia Mosore leo Ijumaa Julai 13, 2018 ametangaza kurejea CCM.
Akizungumza na waandishi wa habari Mosore amesema aliamua kuhama CCM kwa kuwa utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho haukuwa wa kuridhisha.
Akiwa na wanachama wengine watano wa NCCR waliohamia CCM, Mosore ametaja sababu nyingine kuwa ni rushwa na ukosefu wa maadili, akidai kuwa zilikuwa hoja kuu za upinzani lakini kwa sasa zinatekelezwa ipasavyo na Serikali ya Awamu ya Tano.
“Kipindi cha uongozi wa Rais John Magufuli kwa miaka hii miwili ameshughulikia kweli kweli suala la rushwa na maadili. Serikali inafanya kazi kwa uwazi, ukusanyaji wa mapato ni mzuri. Pia imedhibiti matumizi yasiyo ya lazima,” amesema.
Wengine waliotangaza kujiunga na CCM ni aliyekuwa mjumbe wa halmashauri kuu ya NCCR, Mchata Mchata; aliyekuwa Katibu Jimbo la Segerea, Lilian Kitunga; aliyekuwa Katibu wa wanawake Segerea, Nossy Chacha pamoja na Vedalin Nicholaus na Eunice Zarcharia.
0 Comments