Atupwa Jela maisha kwa kulawiti watoto Wawili

Atupwa Jela maisha kwa kulawiti watoto Wawili


Mahakama ya Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, imemhukumu kifungo cha maisha jela Mathias Mbaya, mkazi wa Maleza Mkwajuni wilayani Songwe baada ya kupatikana na hatia ya kuwalawiti watoto wawili.


Mahakama hiyo ilitoa hukumu hiyo juzi, kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo na pande zote mbili.


Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Nemes Chami, alisema mahakama imemkuta na hatia mtuhumiwa pasipo kuacha shaka, baada ya ushahidi kutolewa kwa pande zote mbili.


Mbali na ushahidi huo, mshtakiwa pia alikiri kutenda kosa hilo hivyo kuhukumiwa kifungo cha maisha jela, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ya kutenda makosa kama hayo.


Awali, mwendesha mashtaka wa serikali, Peter Miisho, alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kwa nyakati tofauti Mei 23, mwaka huu, katika kijiji cha Maleza wilayani Songwe kwa kuwalawiti watoto wenye miaka mitano na saba.


Alidai kuwa baada ya kutenda unyama huo na kuwasababishia maumivu makali watoto hao, mshtakiwa alikamatwa akiwa katika harakati za kukimbia na kufunguliwa kesi.


Kutokana na kitendo hicho, mwendesha mashtaka huyo aliiomba mahakama itoe adhabu kali, ili iwe fundisho kwa wengine na ndipo hakimu alipotoa kifungo hicho.


Nje ya mahakama, baadhi ya wananchi waliohudhuria wakati wa kutolewa hukumu hiyo, waliipongeza mahakama kwa madai kwamba adhabu hiyo itapunguza vitendo vya kikatili kama hivyo vinavyofanywa dhidi ya watoto.

Post a Comment

0 Comments