KAIMU Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Liberatus Sabas amewataka madereva wote kupeleka leseni zao kwenye vituo vikubwa vya Polisi au Polisi Usalama Barabarani Kanda Maalumu kwa ajili ya ukaguzi.
Agizo hilo lilitolewa na kamanda huyo jana wakati akizindua operesheni ya ukaguzi wa magari, madereva, leseni na vyeti vya udereva katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani na nje ya nchi, Ubungo.
Sabas alisema lengo la operesheni hiyo ni kukagua leseni ili kubaini leseni za kughushi zilizopatikana kwa njia isiyo halali, kubaini vyeti vya udereva ambavyo ni halali ama vya kughushi, kubaini magari mabovu na yasiyofaa kuwepo barabarani kwa kuzingatia ubora wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Alisema katika operesheni hiyo waliyoifanya wapo madereva waliokutwa wana leseni feki, yapo magari ambayo yamekutwa hayana ubora wa kusafirisha abiria, jambo ambalo ni kinyume cha sheria za usalama barabarani.
“Wapo waliokutwa na matatizo ikiwemo kutokuwa na leseni, magari hayana ubora, ni muhimu wakaelewa operesheni hii itaendelea nchi nzima, ninavyozungumza hivi popote walipo madereva na magari yao wajue kwamba watakutana na operesheni hii Mwanza, iwe Kigoma, iwe Mtwara, iwe Lindi, iwe Ruvuma,” alisema.
Alisema matarajio yao baada ya operesheni hiyo ni kuwafanya madereva kuacha tabia ya kughushi leseni, kuwahimiza madereva wajiunge na mafunzo ya udereva katika vyuo vinavyotambulika na serikali.
Pia kujenga mahusiano mazuri kati ya Jeshi la Polisi, wamiliki, madereva na mawakala wa usafirishaji na wamiliki wapate elimu ya ukaguzi wa magari ambao bora ni ule unaozingatia ubora wa tairi.
Pamoja na kuwajengea utaratibu wa kukagua vifaa vyote vilivyo mbele ya gari, vinavyoongoza mfumo wa injini, mfumo wa breki, usukani na mfumo wa umeme na kuhakikisha madereva wote wenye leseni za kughushi au waliozipata kwa njia zisizo halali wanaacha kuendesha.
Sabas aliwataka madereva wasio na leseni halali, madereva walevi, wamiliki wa magari walio na magari mabovu, kutoyaruhusu magari hayo kuingia barabarani hadi yatakapotengenezwa na kukaguliwa.
Pia aliwataka wamiliki wote wa magari, madereva na watumiaji wengine wote wa barabara, kuchukua tahadhari za kiusalama kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usalama barabarani wakati wote ili kupambana na ajali zinazoweza kuzuilika.
“Jeshi la Polisi halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wamiliki, madereva na kampuni za usafirishaji zitakazokwenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani,” alisema Sabas.
Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Dar es Salaam, Marison Mwakyoma alisema kuwa operesheni hiyo imekuja baada ya kugundua kuwa baadhi ya madereva, wana leseni feki pamoja na ukosefu wa elimu kwa madereva ambapo wengi wao wanaogopa askari wa usalama barabarani badala ya kuogopa sheria.
“Tunataka watu waogope sheria wasiogope trafiki, asilimia kubwa ya madereva wanaogopa askari wa usalama barabarani na ndio maana akifika njiani anamuuliza mwenzake ‘huko vipi?’ akishamwambia kupo salama anapita anaendesha mwendo,” alisema Mwakyoma.
0 Comments