Mwanasiasa wa upinzani aachiliwa huru kwa dhamana

Mwanasiasa wa upinzani aachiliwa huru kwa dhamana


Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa amesema mwanasiasa wa upinzani Tendai Biti ameachiliwa huru na mahakama baada ya yeye kuingilia kati.

Akiandika katika mtandao wa Twitter, kiongozi huyo wa Zimbabwe ametaka kuwepo kwa amani.

Lakini amesisitiza kuwa taratibu zaidi za kisheria zitafuata mkondo wake.

Bwana Biti alikamatwa baada ya kushutumiwa kuutangazia umma wa Zimbabwe kuwa chama cha upinzani MDC kimeshinda uchaguzi wa hivi karibuni, kitendo ambacho kinatajwa kuchochea vurugu kwa wananchi.

Biti ambaye alirejeshwa nchini Zimbabwe baada ya kujaribu kuingia Zambia, ni mwanasiasa wenye ushawishi mkubwa na waziri wa zamani wa fedha kwenye serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa na Rais wa zamani Robert Mugabe na aliyekuwa waziri mkuu hayati Morgan Tsvangirai.



Kurejeshwa kwake kulifuatia agizo la mahakama la kumtafuta popote alipo, baada ya tamko alilolitoa la ushindi wa chama cha upinzani kwenye uchaguzi mkuu uliomaliika hivi majuzi na kumuweka madarakani mwanasiasa mkongwe Emmerson Mnangagwa.

Seneta wa chama cha MDC David Coultart ameiambia BBC kuwa bwana Biti aliteswa wakati wa utawala wa rais wa zamani Robert Mugabe, na kwa sasa anahofia usalama wake hivyo ni vyema mahakama hata baada ya kumuachia impe ulinzi.

Awali mwanasheria wa Biti alisema maisha ya mwanasiasa huyo yapo hatarini nchini Zimbabwe kauli ambayo ilikanushwa vikali na waziri wa mamambo ya nje wa Zambia Joseph Malanji akisema serikali yake haiamini kama Biti anaweza kuwa katika hatari ndani ya nchi yake mwenyewe.

Post a Comment

0 Comments