Wamiliki ving'amuzi waongeza machungu

Wamiliki ving'amuzi waongeza machungu



KAMPUNI zinazomiliki minara ya kurusha matangazo ya televisheni zimetoa siku 30 kwa wamiliki wa vituo vya televisheni nchini kulipa gharama za kila mwezi vinginevyo zitaondolewa katika minara hiyo.

Kampuni hizo za minara zimesema televisheni za ndani kwa muda mrefu zinapatiwa huduma hiyo bila kulipia, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Zimesema utaratibu uliowekwa kisheria unawataka wamiliki wa kituo cha televisheni kulipa Sh. milioni 2.4 kwa mwezi kwa kila mkoa au kanda ambayo inapata matangazo ya kituo husika.

Wawakilishi wa kampuni za Agape, Star Media na Basic Transmission, waliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam walipozungumza na waandishi wa habari.

Katika mkutano huo, Mch. Vernon Fernandos, mwakilishi wa kampuni ya Agape, alisema kuwa tangu mwaka 2010, televisheni za ndani (local channels) zimegoma kulipa gharama za kurusha maudhui yake.

Alisema katika kipindi chote, sheria ilikuwa inazitaka televisheni za ndani kulipia gharama za kurusha maudhui, lakini hilo halikufanyika kwa miaka nane sasa.

"Tunatoa mwezi mmoja kwa televisheni zote kulipa gharama za kurusha maudhui wanayoandaa na baada ya kipindi hicho kumalizika, wakigoma kulipa tutakaa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano (TCRA) na wamiliki wa televisheni hizo na kuziondoa zisionekane," alisema.

"Baada ya kuondolewa kuonyeshwa bure, itamlazimu mtumiaji wa mwisho ambaye ni mwananchi anunue king'amuzi cha kampuni hizo, ili kupata matangazo ya televisheni hizo."

Alisema hadi sasa kampuni hizo tatu zina minara 47 ya kurusha matangazo kwa nchi nzima inayotumiwa na televisheni za ndani 34.

Aliongeza kuwa kila televisheni ina leseni ambayo inaonyesha inatakiwa kurusha matangazo katika eneo gani na la ukubwa gani.

Kwa mujibu wa Fernandos, televisheni za kitaifa ambazo zinaonekana mikoa yote pia zitatakiwa kulipa gharama kulingana na ukubwa wa eneo ingawa alisema bado kuna nafasi ya mazungumzo ili kuwapunguzia bei ya kurusha kwa kila mwezi.

Kwa upande wake, mwakilishi wa Kampuni ya Star Media, Justin Ndege, alisema kwa muda wa miaka nane wamekuwa wakipata hasara kwa kuwa televisheni za ndani zimegoma kulipa.

Alisema kampuni hizo zimetumia mtaji mkubwa katika uwekezaji na wanaona sasa ni wakati mwafaka kwa televisheni hizo kulipa gharama kwa mujibu wa sheria.

WIZARA YAJITOSA

Wakati hayo yakijitokeza, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imesema itaingilia kati mvutano uliopo kati ya TCRA na kampuni zinazorusha chaneli za televisheni nchini.

Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, alisema mkoani Pwani jana, kuwa wizara yake inalichukulia umuhimu suala hilo kwa kuwa ni la biashara na uwekezaji.

Katika ziara ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kwenye kiwanda cha kuchakata matunda na vinywaji baridi cha Kampuni ya Bakhresa mkoani Pwani, Manyanya alisema watahitaji kujua zaidi na kuona suala hilo linapatiwa ufumbuzi wa haraka.

"Sisi tunalichukulia suala hili kama la biashara, tutapenda kulifahamu zaidi…je, TCRA na wamiliki wa ving'amuzi hawawezi kukaa pamoja na kutatua tatizo hili? Sisi ni viwanda, biashara na uwekezaji, hivyo kuna uwekezaji na biashara hapo na tuna wajibu wa kulifuatilia," alisema.

Aliwataka wamiliki wa ving'amuzi nchini kutokuwa na mazoea ya kukimbilia mahakamani kwa kuwa suala kama hilo linazungumzika.

"Tunaamini bila nyie nchi haiwezi kwenda na tunapenda Watanzania wapate habari, pia nina hakika serikali ni sikivu na imekuwa ikitatua kero nyingi zinazogusa Watanzania, hivyo hata suala hili litapatiwa ufumbuzi karibuni," alisema.

Mjumbe wa kamati hiyo na Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Tabora, Hawa Mwaifunga, alitaka ufafanuzi kutoka kwa uongozi wa Kampuni ya Azam Media kuhusu kuzuiwa kwao kurusha chaneli za ndani kupitia king’amuzi cha Azam TV.

"Mimi naomba kujua na kupata sababu nini kilitokea hadi mmezuiliwa kurusha chaneli za ndani?" Mwaifunga alihoji.

Akijibu swali hilo, Mkuu wa Uhusiano na Masuala ya Ndani wa Kampuni ya Bakhresa Group, Hussein Sufiani, alisema chanzo cha zuio hilo ni mabadiliko ya sheria.

Alisema kuna haja kwa serikali kupitia upya na kuzifanyia marekebisho sheria ili ziendane na wakati uliopo.

"Kama sheria mpya hazitambui sheria za zamani, basi kuna haja zibadilishwe ili ziendane na za sasa," Sufiani alisema.

Wiki iliyopita, TCRA ilitishia kuzinyang'anya leseni kampuni za Multichoice Tanzania Limited na Simbanet Tanzania Limited kwa kukiuka masharti ya leseni zake kurusha maudhui ya nje na kuuza maudhui ya ndani kwa muundo wa malipo ya kabla.

Post a Comment

0 Comments