HAIJAWAHI Tokea…Kishindo cha Rais Magufuli Migodini Chalipa

HAIJAWAHI Tokea…Kishindo cha Rais Magufuli Migodini Chalipa



KISHINDO cha Rais John Magufuli kuzuia kusafirishwa nje ya nchi mchanga wa madini maarufu kama ‘makinikia’ kisha kupeleka bungeni miswada mitatu kwa lengo la kubadili sheria ili kunufaisha taifa, kimeanza kuzaa matunda baada ya kuungwa mkono hadi ughaibuni.

Hali hiyo imetokana na mabilionea wa kampuni mbili za Australia na Canada zenye kujihusisha na shughuli za madini nchini kueleza namna zinavyomuunga mkono Magufuli (maarufu JPM), huku pia zikimpongeza na kuita hatua alizochukua kuwa ni za kizalendo.

Hivi karibuni, Magufuli aliunda kamati mbili zilizochunguza usafirishaji wa makinikia kwenda ughaibuni ambazo ripoti zake zilifichua upotevu mkubwa wa mapato kwa taifa.

Aidha, kutokana na matokeo ya ripoti hizo na mapendekezo yaliyotolewa, Serikali ilipeleka bungeni miswada mitatu iliyopitishwa kwa kishindo kuridhia mabadiliko kadhaa ya sheria, lengo likiwa ni kulinufaisha taifa na rasilimali tele ilizojaaliwa na siyo wawekezaji pekee.

Juni 29, mwaka huu, serikali iliwasilisha bungeni miswada mitatu inayohusu rasilimali za nchi ukiwamo muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa mwaka 2017, Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano kuhusu Masharti hasi katika Mikataba ya Maliasili za nchi wa mwaka 2017, na Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi kuhusiana na Umiliki wa Maliasili wa mwaka 2017.

Katika taarifa iliyochapishwa jana na gazeti dada la Nipashe la The Guardian, Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni ya Royalty Exploration ya Canada inayofanya kazi zake nchini, James Sinclair, alisema uamuzi wa serikali wa kuwasilisha miswada kwa hati ya dharura bungeni ili kubadili sheria mbovu zilizopo ni hatua ya kupongezwa.

“Mapendekezo ya mabadiliko ya sheria yanalenga kuleta usawa katika rasilimali zinazopatikana nchini lakini tunaamini sheria hizo hizo pia zitaweka vitu vitakavyowavutia wawekezaji,” alisema.

Kampuni ya Tanzania Royalty Exploration Corporation, yenye makao makuu Toronto, Canada, inamiliki asilimia 55 ya hisa katika mradi wa Buckreef Gold Mine nchini na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) linamiliki asilimia 45.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Sinclair akiwa nchini Canada, kampuni yake ya Buckreef Gold inaunga mkono mabadiliko hayo ya sheria yanayokusudiwa kufanyika nchini.

Aliwahakikishia wanahisa wake kuwa kupitishwa kwa miswada hiyo na hatimaye kuwa sheria baadaye hakutaathiri uendeshaji wa kampuni hiyo.

Alisema dhamira yake ni kushiriki kwenye maendeleo ya uchumi wa mataifa ya kigeni katika misingi ya usawa kwenye mikataba inayoingiwa.

Katika miswada iliyopitishwa bungeni wiki hii, serikali imeongeza tozo ya mrabaha kwenye dhahabu, fedha, shaba na platinum kufikia asilimia sita kutoka iliyokuwa asilimia nne na kupandisha hisa za serikali kwenye umiliki wa kampuni za madini kufikia asilimia 16.

Nayo Kampuni ya Australia ya Cradle Resources, ilisema kwenye taarifa yake kuwa mabadiliko ya sheria yatokanayo na miswada iliyopitishwa bungeni hayawezi kuwaathiri kwa kiasi kikubwa, ingawa mpango wake wa kutoa dola za Marekani milioni 55 zilizokuwa zimependekezwa zichukuliwe na wabia wake Kampuni ya Tremont Investments, umezimika kutokana na mabadiliko hayo.

Kampuni mbili zilizoko kwenye Soko la Hisa la Australia (ASX), zilisema kwenye taarifa yao kuwa zina imani kuwa uwekezaji wanaoufanya nchini Tanzania utakuwa wa manufaa licha ya mabadiliko hayo ya sheria za madini.

Walkabout Resources Limited ya Australia, ilisema mabadiliko hayo hayawezi kusababisha athari mbaya kwenye uendeshaji wa shughuli zao.

Ilisema kwa kushirikiana na wanasheria wa ndani na wa nje walifanyia upembuzi wa miswada iliyopitishwa na Bunge na kubaini kuwa itakuwa na manufaa hata kwenye mradi wake wa Lindi Jumbo.

“Tumepitia kwa makini mabadiliko hayo, tumeangalia athari zake kwenye miradi yetu na baada ya kusikiliza maoni ya wanasheria wa ndani na wa nje ya kampuni hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika ambayo yatasababisha kampuni kupunguza au kusitisha uwekezaji wake nchini Tanzania,” ilisema taarifa hiyo.

Chanzo: Nipashe

Post a Comment

0 Comments