Dar es Salaam. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imewataja vigogo wa serikali, wanasiasa na viongozi wa dini watatu walionufaika na uchotwaji wa Sh306 bilioni katika Akaunti ya Tegeta Escrow na jinsi baadhi walivyotumia mifuko ya plastiki kuzibeba.
Akisoma maoni ya kamati hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zitto Kabwe aliwataja waliochukua fedha hizo kutoka kwa mkurugenzi wa VIP, James Rugemalira na kiwango walichopokea katika mabano kuwa ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge (Sh1.6 bilioni) na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka (Sh1.6 bilioni).
Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ambaye pia ni mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (Sh40.4 milioni), aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh40.4 milioni), Mbunge mstaafu wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh40.4 milioni), aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk Enos Bukuku (Sh161.7 milioni).
Alisema majaji walioingiziwa fedha ni Jaji Profesa Eudes Ruhangisa (Sh404.25 milioni) na Jaji A.K Mujulizi (Sh40.4 milioni).
Kwa upande wa watumishi wa umma, Zitto alisema kuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usajili wa Vizazi na Vifo (Rita), Philip Saliboko (Sh40.4 milioni), aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emmanuel Daniel Ole Naiko (Sh40.4 milioni) na ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Lucy Appollo (Sh80.8 milioni).
Askofu Kilaini atajwa
Zitto alisema, “Kwa upande wa viongozi wa dini ambao waliingiziwa fedha na Benki ya Mkombozi ni Askofu Methodius Kilaini (Sh80.9 milioni), Askofu Eusebius Nzigirwa (Sh40.4 milioni) na Padri Alphonce Twimannye Simon (Sh40.4 milioni).
Aliongeza, “Kamati ya PAC ilithibitishiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru kuwa baadhi ya watu walienda kugawana fedha kwenye benki tajwa (Mkombozi) wakiwa na mifuko ya rambo, sandarusi, maboksi, magunia na lumbesa.”
Mkurugenzi Rugemalira
Zitto alisema Mkurugenzi Mtendaji wa VIP Engeneering, James Rugemalira alipata mgawo wa Dola za Marekani Sh75 milioni kutoka katika fedha zilizokuwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow na kuzigawa kwa watu mbalimbali.
Rugemalira ambaye alikuwa na hisa 3 kati ya 10 za kampuni ya IPTL, alichukua kiasi hicho cha fedha na kukipeleka katika Benki ya Mkombozi inayomilikiwa na Kanisa Katoliki.
Zitto alisema Rugemalira alionekana kuhusika na IPTL pale alipofungua shauri mahakamani kuomba kuiondoa IPTL kwenye ufilisi na kisha kuuza hisa zake kwa kampuni ya PAP.
Alisema baada ya uamuzi wa Kahakama Kuu kutolewa Septemba 5, 2013, fedha za Escrow zilitolewa kwa haraka na kupelekwa katika benki hiyo baadaye kugawiwa kwa vigogo hao.
Kamati hiyo imekabidhiwa taarifa za Benki za Stanbic na Mkombozi ambazo zimeonyesha namna ambavyo fedha zilichukuliwa na watu na kampuni mbalimbali.
Ripoti hiyo ya PAC iliyosomwa jana ilikuwa na kurasa 116 na maneno 16,979.
0 Comments