Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuiona siku nyingine tena. Ni kitu cha kwanza nilichokisema wakati naamka, nikatafuta simu yangu nilipoiweka na kuanza kuangalia mitandaoni habari mpya zinazoendelea – Nimeshtuka sana kuona mjadala unaoendelea ni kuhusu video mpya ya Diamond ‘Eneka’.
Ndio kwanza video hiyo ina siku takribani tatu au nne tangu imewekwa kwenye mtandao wa YouTube, lakini kwa mjadala wake umezidi kuwa mkubwa zaidi kila kukicha lakini kwa msanii mwenyewe hilo ni jambo zuri kwa upande wake kwa kuwa inazidi kuufanya wimbo wake uzidi kutembea na hata wale ambao hawajauona watatamani kuutafuta ili kufahamu zaidi kile kinachozungumziwa.
Nimewakumbuka wahenga walisema “Usiache mbachao kwa msala upitao,” na mimi jambo hili nimeshindwa kulivumilia na nimeamua kuweka japo neno kwenye huu mjadala wa kuweza kutazama kama unaweza kufika mwisho.
Ni kweli vitu kama viwili kwenye video ya ‘Eneka’ vinafanana na video mbili tofauti, ya kwanza ni ile ya wasanii wa Ghana, R2Bees ‘Tonight’ waliomshirikisha Wizkid. Video hizi mbili zinafanana kutokana na location moja ya jangwani ambapo gari likiwa linatembea ambapo magari yote mawili yaliyotumika katika video hizo yanafanana rangi moja ambayo ni nyekundu. Hata hivyo sishangai kwa hilo kwa kuwa video hizi zote mbili zimeongozwa na director mmoja Sesan Ogunro kutoka Nigeria.
Na video ya pili ni ‘My Lilly’ ya Jah Prayzah aliyomshirikisha Davido. Zote mbili zinaonyesha kufanana kwenye location ya jumba moja ambapo kuna sehemu wasanii hao wakiwa wanaimba nyumba yake kuna maji yanaonekana kumwagika. Lakini nimebakiwa na swali ambalo nimekosa majibu yake, kama video hizi zimepishana siku mbili ni nani alikuwa wa kwanza kushoot katika eneo hilo? Na kwanini watu wanamlenga Diamond ndio kaiga location wakati hajawahi kuposti picha au kutangaza kuna video ya Eneka anakuja nayo mpaka pale alipoiachia kwa surprise ndio watu wakajua kama kulikuwa na mzigo huo kwenye store yake.
Hataka kama hilo limetokea lakini hakuna dhambi kwenye hilo iliyotendeka. Kwa nini tunakuwa wavivu wa kufikiria kwenye hili na kuwa wepesi wa kusahau mambo yaliyopita muda mfupi, na kwanini kila siku Diamond kila anapoachia video mpya au kufanya lolote hawezi kupokea majibu positive lazima kuwe na negative? Kwa hapa hata kama adui yako muombee njaa lakini tusisahau kuwa kizuri kisifiwe pia.
Naomba nikukumbushe video hizi nyingine ambazo zilirudia location ya jengo moja lililopo huko Afrika Kusini lakini hakuna kilichozungumzwa zaidi na watu kupotezea kama hawajui zaidi ya kusikia Diamond tena akitajwa kwenye hilo na kuwasahau wengine.
Runtown – Walahi, video hii imewekwa kwenye mtandao wa YouTube Novemba 2, 2015 na imeongozwa na director Sesan kutoka Nigeria.
Diamond – Utanipenda, imeongozwa na Godfather na imewekwa kwenye mtandao wa YouTube Dec 11, 2015.
Wizkid – Baba Nla, video hii imewekwa kwenye mtandao wa YouTube Disemba 10, 2015 na imeongozwa na Sesan.
Brown Mauzo f/ Alikiba – Nitunzie, imeongozwa na director Nicorux na imewekwa kwenye mtandao wa YouTube Septemba 20, 2016.
0 Comments