TUCTA Yawatoa Hofu Watumishi Wenye Vyeti FEKI

TUCTA Yawatoa Hofu Watumishi Wenye Vyeti FEKI


Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limewatoa hofu watumishi wa Serikali waliokutwa na vyeti feki na kuwataka kupuuza taarifa kuwa hawatolipwa malimbikizo ya madai yao.

Limewahakikishia watumishi hao, wanaoidai Serikali malimbikizo mbalimbali kuwa mchakato wa ulipaji wa malimbikizo yao ya mishahara na madai mengine utaanza hivi karibuni.

Kauli hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu makubaliano waliyoafikiana na Serikali.

“Kumekuwapo na taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa watumishi waliokutwa na vyeti feki hawatolipwa madai yao, jambo hilo si kweli, nawahakikishia watumishi hawa TUCTA tumekutana na waziri mwenye dhamana na katibu mkuu wake ambao nao wamesema taarifa hizi hazina ukweli.

“Tumeambiwa uhakiki utakapokamilika, ndipo watatangaza uamuzi wa madai yao,” alisema.
Kuhusu malimbikizo ya mishahara na madai mengine ya watumishi wa Serikali, wakiwamo walimu, Nyamhokya alisema wamehakikishiwa wataanza kulipwa hivi karibuni.


“Ingawa hatukupewa muda kamili yataanza kulipwa lini, niwatoe hofu watumishi kuwa madai yao yote yataanza kulipwa hivi karibuni… kauli ambayo imetoka kwa waziri mwenyewe, baada ya kukutana naye ana kwa ana ofisini kwake hivi karibuni,” alisema.


Licha ya kupongeza juhudi za Rais Dk. John Magufuli katika kuisafisha Serikali, Nyamhokya aliiomba Serikali kutekeleza ahadi za rais alizozitoa wakati akihutubia sherehe za Mei Mosi, mwaka huu.


“Aliahidi kurejesha madaraja kwa wafanyakazi katika mwaka huu wa fedha, kuongeza mishahara pamoja na kulipa madeni ya watumishi wote,” alisema.


Hadi kufikia Novemba, mwaka jana, Serikali imelipa Sh bilioni 29 kwa watumishi mbalimbali wa umma wakiwamo walimu.


Hata hivyo, kwa mujibu wa hotuba aliyotolewa bungeni Aprili 18, mwaka huu na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora), Angellah Kairuki, ni madai 18,823 ya malimbikizo ya watumishi yenye thamani ya Sh bilioni 32.8 ambayo yamehakikiwa na kuingizwa kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mshahara kwa malipo.

Post a Comment

0 Comments