Wakati Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli imejipambanua kuongeza vitega uchumi kama vile ununuzi wa ndege mpya aina ya bombardier, Chadema wameibuka na uchambuzi wa hali ya uchumi na kudai hali sasa ni tete ukilinganisha na awamu iliyopita.
Jana, Chadema ilitoa tamko la tathmini ya hali ya uchumi nchini baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kukutana kwa dharura kwa siku mbili mfululizo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na wanahabari, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe alisema tamko hilo limejikita katika ripoti ya hali ya uchumi inayotolewa kila mwezi na Benki Kuu Tanzania (BoT) kama ilivyotolewa Julai 14, 2017.
Alisema Julai 14, BoT ilitoa ripoti ya Juni inayohusu tathmini ya Mei.
Kwa kuzingatia umuhimu wake, alisema Chadema imefanya uchambuzi wa ripoti hiyo kwa kuangalia hali ya uchumi mpaka kufikia Mei 2017 ikilinganishwa na hali ya uchumi iliyokuwapo Mei 2015 ikiwa ndio mwaka wa mwisho wa Awamu ya Nne ili kuona mwelekeo wa hali ya uchumi na athari zake chanya au hasi kwa mustakabali wa Taifa.
Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu madai ya Chadema kuhusu kuporomoka kwa uchumi wa Tanzania, Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu hakuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kwamba yuko kijijini na hajui kinachoendelea.
“Mimi nataka nikiongelea kitu niwe ninakifahamu vizuri, hilo suala sijalisikia kwa hiyo siwezi kusema chochote kupitia mtu wa tatu,”alisema Profesa Ndulu akisisitiza kwamba kwa sasa hayupo ofisini.
Lakini, Mbowe ambaye aliambatana na viongozi waandamizi wa chama hicho akiwamo Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji na Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward Lowassa alisema uchumi hupimwa kwa vigezo vingi na umuhimu wa vigezo husika huwa na maana kutegemeana na namna vinavyoathiri maisha ya wananchi. Katika uchambuzi wao, waliangalia vigezo vichache ambavyo vina uhusiano wa moja kwa moja kwenye maisha ya wananchi.
Mbowe alisema kwa kipindi cha Mei, 2015 kiasi cha akiba ya chakula kwenye Ghala la Taifa (NFRA) kilifikia tani 406,846 ukilinganisha na akiba ya tani 74,826 ilipofika Mei 2017, sawa na asilimia 18.3 tu ya kiasi cha chakula katika kipindi kama hicho mwaka 2015.
“Bei za jumla kwa vyakula muhimu kama mahindi, Mei 2015 ilikuwa Sh47,163 kwa gunia wakati mwaka huu mwezi kama huo ilifikia Sh90,149.9 sawa na ongezeko la bei kwa asilimia 92 wakati mchele gunia mwaka 2015 ilikuwa Sh162,701 na mwaka huu mwezi kama huo ilifika Sh176,330,” alisema Mbowe.
Mwanasiasa huyo aliongeza kuwa mazao mengine yote ya chakula ikiwamo maharage, viazi na sukari nayo yamepanda bei kwa wastani wa asilimia kati ya 40 na 60 kutegemea na msimu.
Mbowe alisema kuwa sekta hiyo imekua kwa asilimia 1.7 pekee mwaka 2016/17, kiwango ambacho ni cha chini kupata kutokea kwa zaidi ya miongo mitatu.
“Wakati mataifa yote duniani yanasaidia wakulima kuongeza tija katika kilimo kwa kuwasaidia ruzuku ya mbolea, Tanzania ambayo asilimia 75 wanategemea kilimo mwaka 2015 ilikuwa Sh78 bilioni wakati mwaka 2016/17 ruzuku hii ilikuwa Sh10 bilioni tu,” alisisitiza Mbowe.
Alisema kwa upande wa tume ya maji iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria 2015 kwa lengo la kuhakikisha wanaongeza kilimo cha umwagiliaji katika bajeti ya mwaka 2016/17, ilipata Sh 0 (sifuri) katika bajeti yake ya maendeleo.
Mwenyeiti huyo ambaye aliwahi kugombea urais kwa tiketi ya chama chake na kushindwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisema wakati bei zikiwa juu sasa kuliko mwaka 2015 kabla ya Awamu ya Tano kuingia madarakani, hali ya ujazo wa fedha imekua kinyume chake na hivyo kuathiri biashara, uzalishaji, thamani ya mali kama ardhi huku ujazo wa fedha katika dhana pana kwa mwaka kwenye uchumi uliongezeka kwa asilimia 15 Mei 2015 ukilinganisha na ongezeko la asilimia 5.2 Mei mwaka huu.
Alisema kwa upande wa mzunguko wa fedha kwa maana ya kiasi cha fedha katika matumizi kwa mwaka, inaonyesha Mei 2015 kiliongezeka kwa asilimia 15.2 wakati 2017 kilikuwa na ongezeko hasi kwa asilimia tatu.
“Hiki ni kielelezo cha usimamizi hafifu wa uchumi na ndio msingi wa ukata unaoendelea nchini.”
Alisema athari za kushuka kwa ujazo wa fedha na mzunguko wa fedha kwenye uchumi katika vipindi hivyo tofauti wakati kiasi cha mfumuko wa bei kikiwa na tofauti ndogo, kwa maana kutoka asilimia tano mwaka 2015 mpaka asilimia sita 2017 ni pamoja na fedha kuwa vigumu kupatikana japo inashuka thamani.
“ Ndio maana pamoja na mwaka 2017 fedha kuwa ngumu kuliko mwaka 2015 kwa mujibu wa takwimu hizi za BoT, lakini thamani ya bei ya chakula kama mahindi na maharage vimepanda karibu mara mbili kwa ulinganisho wa miaka hiyo miwili,” alisisitiza.
Mwenyekiti huyo alisema pia kuwa gharama ya uzalishaji kwa sehemu kubwa inabaki kuwa juu kwa sababu bidhaa za mtaji na mashine sehemu kubwa zinanunuliwa nje na hivyo bei yake haiamuliwi na hali ya ndani kwa sababu wateja kipato kimeshuka, soko la bidhaa zinazozalishwa hushuka na kusababisha mdororo wa biashara.
Alisema kwa sababu ya mdororo wa biashara, wafanyabiashara wanashindwa kulipa mikopo na hivyo kuongeza presha kwenye kasi ya mikopo isiyolipika (non performing loans -NPL).
Alisema mpaka sasa kwa mujibu wa ripoti mbalimbali mikopo isiyolipika imeongezeka kutoka chini ya asilimia tano mwaka 2015 mpaka asilimia zaidi ya nane mwaka 2017 jambo alilodai kuwa linapunguza imani ya benki za biashara kukopesha sekta binafsi.
Alisema ukata huo unasababisha kushuka kwa thamani ya mali kama ardhi, nyumba au mashine na mitambo iliyowekwa dhamana benki kwa ajili ya kupata mikopo kwa sababu uwezo wa watu kununua umeshuka.
“Ndiyo sababu viwanja ambavyo viliuzwa Sh100 milioni sasa ukitangaza bei ya Sh50 milioni hupati mteja, gari au mashine ambayo mwaka 2015 ungeuza kwa Sh50 milioni leo huwezi kupata nusu yake kwa sababu ya ukata.”
Alisema pia uwezo wa Serikali na watu kujitegemea unapungua kwa sababu wigo wa makusanyo unapungua kutokana na biashara nyingi na ajira kupotea.
“Kwa sababu hiyo, maamuzi ya kisera na kisheria ya kushinikiza kampuni za simu zilizoorodheshwa soko la mitaji (DSE) yamekuwa na mafanikio hafifu hata kuhitajika kubadilisha sheria kwa sababu sera mbovu za kiuchumi zimepunguza uwezo wa Watanzania kutumia fursa hizo kuwekeza. Ndio sababu majuzi kampuni ya Vodacom imejaribu kuongeza muda kuwa ipo pamoja na sasa kuruhusu wasio wazawa kununua hisa hizo,” alisema mbunge huyo wa Jimbo la Hai.
Serikali Yajibu Mapigo
Akizungumzia tuhuma za Chadema kuhusu hali ya uchumi, Msemaji wa Serikali, Dk Hassan Abbas alihoji tuhuma hizo kwamba haziendani na hali halisi ipi wakati wanafunzi wanasoma bure hadi kidato cha nne?
Dk Abbas aliwashangaa Chadema kwa kusema; “hawaoni miradi mikubwa ya ujenzi inayoendelea kama vile barabara, mradi wa umeme wa Kinyerezi II Dar es Salaam, flyover ya Tazara na ununuzi wa ndege.
“Serikali inaajiri wafanyakazi wapya; inalipa mishahara kwa wakati; miradi ya maji inaendelea nchi nzima ikiwemo mikubwa ya kutoa maji Ziwa Victoria,” alifafanua Dk Abbas.
Alisema Serikali imeongeza makusanyo ya mapato na imeongeza bajeti katika huduma za jamii, kama vile afya hasa kwenye ununuzi wa dawa. Na kwamba hata wabunge wa Chadema wakiwa bungeni wanalipwa posho zao kama kawaida.
“Wanataka uhalisia upi zaidi ya ushahidi huu kuwa uchumi wa nchi unafaidisha wananchi kupitia huduma hizo?" alihoji Dk Abbas .
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole yeye alisema chama chake hakina muda wa kulumbana na kwamba sasa wana kazi ya kuwaletea maendeleo wananchi.
“Sisi tuna mkataba na wananchi wa Tanzania kuhakikisha tunawaletea maendeleo, kwa sasa tupo ‘busy’ kufanya kazi hiyo, kiukweli hatuna muda wa kufanya malumbano yasiyo na tija, tunachojua ni kazi kubwa iliyopo mbele yetu ambayo tumesaini mkataba mpaka mwaka 2020.”
“Hatuna muda wa kuhangaika na watu wasio na dhamira njema, tunaendelea na kazi na matunda yake yatawanufaisha wananchi wa kawaida kabisa ambao ni wakulima, wafanyabiashara na wafanyakazi. Sisi hatuna muda wa kupoteza,”alisisitiza Polepole
0 Comments