Waziri Mkuu amkabidhisha kwa TAKUKURU aliyekuwa Meya Mbeya

Waziri Mkuu amkabidhisha kwa TAKUKURU aliyekuwa Meya Mbeya


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Mbeya, Emanuel Kiabo kumkamata na kumuhoji aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya Atanas Kapunga na wenzake 11 kwa tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 63.448.


Waziri Mkuu ametoa agizo hilo Jumatatu hii alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za wilaya ya Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano uliofanyika ukumbi wa Benjamin Mkapa.

“Serikali hii haiwezi ikawaacha watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa halmashauri moja. Kama wako humu ndani naagiza wakamatwe na waanze kuhojiwa na ambao wamestaafu au kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe popote walipo ili nao waje kuhojiwa,” aliagiza Waziri Majaliwa.

Wengine ni waliowahi kuwa wakurugenzi wa Jiji hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi. Elizabeth Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi ya Ukurugenzi.

Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji, Bw. James Jorojik pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni Bw. Mussa Mapunda, Bw. Samweli Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi. Lydia Herbert na Bw. Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya mradi huo bila ya kuzingatia maslahi ya Jiji pamoja Emily Maganga ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa kuwa wameisababishia serikali harasa kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko la Mwanjelwa Jijini Mbeya ambalo hadi sasa halijaonyesha tija.

Post a Comment

0 Comments