TALGWU kumburuza Mkurugenzi Kilosa Mahakamani.

TALGWU kumburuza Mkurugenzi Kilosa Mahakamani.


Chama Cha Wafanyakazi wa Serikali za mitaa (TALGWU) mkoani Morogoro kimedhamiria kumburuza mahakamani Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa kwa kusitisha mishahara ya wafanyakazi kinyume na utaratibu.
Katibu wa TALGWU mkoani Morogoro, Lawrence Mdega, amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wanachama wao ambao ni watendaji wa kata na vijiji ambao wamenyimwa mishahara ya Julai mwaka huu wakidaiwa kuwa na elimu ya msingi.

"Waziri wa Tamisemi ameagiza watumishi wote wenye elimu ya msingi walioajiriwa kuanzia Mei 20, 2004 waondolewe kazini. Sasa hawa walijiriwa Mei 1, 2004, kwa nini waondolewe?" amehoji Mdega.

Katibu huyo amesema chama kimeshaandika barua kwa Mkurugenzi kutaka watumishi hao wapewe mishahara ya Julai na waendelee kufanya kazi kwani agizo la Waziri haliwahusu.

Mdega amesema wamepokea malalamiko toka kwa wafanyakazi zaidi ya 200 toka halmashauri tano kati ya tisa za mkoa wa Morogoro. Kati ya hao 80 wanatoka Kilosa.

"Tutakwenda kuwatafutia wafanyakazi hawa wa Kilosa haki mahakamani kwani swala lao lipo wazi kabisa maana agizo linasema waondolewe walioajiriwa kuanzia Mei 20. Sasa kwa nini wawaondoe walioajiriwa Mei Mosi?" amehoji Mdega.

Amesema malalamiko ya wilaya nyingine ameshawasilisha makao makuu ya TALGWU ili washughulikie lakini suala la Kilosa litshughilikiwa na mkoa.

Akizungumzia zoezi hilo, aliyekuwa Mtendaji wa Kata ya Kimamba wilayani Kilosa, Mashaka Motile, amesema katika wilaya hiyo watumishi zaidi ya 80 wamenyimwa mshahara bila maelezo yoyote na walipofuatilia ndipo walipofahamishwa kuwa walipewa muda wa kujiendeleza na wameshindwa kufanya hivyo.

Post a Comment

0 Comments