Waziri Tizeba azidisha idadi wajumbe Bodi ya Kahawa

Waziri Tizeba azidisha idadi wajumbe Bodi ya Kahawa


Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba anadaiwa kukiuka sheria kwa kuteua wajumbe wa Bodi ya Kahawa (TCB) nje ya idadi inayotajwa na Sheria ya Sekta ya Kahawa ya 2001.

Sheria hiyo namba 23 kama ilivyorekebishwa na sheria ya mazao namba 20 ya 2009, imempa waziri mamlaka ya kuteua wajumbe nane lakini katika uteuzi huo, Waziri Tizeba ameteua wajumbe tisa.

Katika jedwali la sheria hiyo kifungu cha 1(1) kinaeleza waziri atateua wajumbe nane tu na Rais atateua mwenyekiti wa bodi baada ya kushauriana na waziri na kufanya bodi nzima kuwa na wajumbe tisa.

Sheria hiyo inataka mjumbe mmoja anapaswa kutoka Tanzania Coffee Association (TCA), mjumbe mmoja kutoka Tanzania Coffee Growers Association (TCGA) na watatu kutoka vyama vya ushirika.

Kwa mujibu wa sheria hiyo, wajumbe watatu kutoka vyama vya ushirika ni lazima watoke katika kanda kubwa zinazozalisha kahawa ambazo ni Kanda ya Kaskazini, Kusini na Kanda ya Ziwa.

Pia, sheria hiyo inataka mjumbe mmoja atoke Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na wajumbe wawili watakuwa ni watu wenye ufahamu na uzoefu katika masuala yanayohusu kilimo cha zao la kahawa.


Hata hivyo, taarifa kwa umma aliyoitoa Dk Tizeba Agosti 10, inaonyesha majina ya watu tisa aliowateua kuwa wajumbe wa bodi ya wakurugenzi ya TCB, idadi ambayo imezidi mtu mmoja kulingana na matakwa ya kisheria.


Taarifa hiyo ya uteuzi iliyotolewa na katibu mkuu wa wizara, Mathew Mtigumwe, haielezi watu hao wanatoka taasisi gani au kanda ipi kama sheria inavyoanisha.


Wajumbe walioteuliwa ni Fatima Faraji, Twahir Nzallawahe, Titus Itigereize, Profesa Faustine Bee, Boaz Mwalusamba, Elizabeth Bwire, Robert Mayongela, Daud Magayane na Amir Hamza.


Awali sheria hiyo ya mwaka 2001 ilitaka Waziri ateue watu sita kuwa wajumbe na mwenyekiti wao ateuliwe na Rais, lakini marekebisho yaliyofuata yaliongeza watu wawili wenye upeo wa mambo ya kahawa.


Alipotafutwa ili azungumzie suala hilo, Waziri Tizeba alisema yuko kwenye mkutano wa CCM hivyo asingeweza kuzungumza.


Lakini, wanasheria waliohojiwa na gazeti hili jana, walisema Waziri Tizeba hakushauriwa vizuri na wataalamu wake kabla ya kufanya uteuzi.


“Wajumbe wanane tu ndio halali kwa mujibu wa sheria na mmoja sio halali chini ya sheria hiyo,” alisema Frank Mushi ambaye ni wakilki wa kujitegemea.


“Sheria iko wazi kuwa wajumbe ni tisa na miongoni mwao atakuwapo mwenyekiti atakayeteuliwa na Rais, tena imetumia neno shall (lazima) mwenyekiti ateuliwe na Rais wa Jamhuri,” alisema.


“Waziri alizidisha powers (madaraka) zake kwa sababu hana mamlaka ya kuteua wajumbe wote tisa isipokuwa wale nane tu. Mahali sheria inapomtaja Rais hapawezi kuwa Waziri.


“Ina maana Rais leo akiteua mwenyekiti, bodi itakuwa na wajumbe 10 ambao ni kinyume cha sheria.” Lakini makamu mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Kahawa cha Kilimanjaro (KNCU), Hatibu Mwanga aliangalia zaidi uwakilishi.


“Sheria inataka waziri ateue wajumbe watatu kutoka vyama vya ushirika katika kila kanda inayolima kahawa, lakini katazame yale majina hakuna mjumbe anayetoka kanda ya kaskazini,” alisema.


Mwanga alisema huwezi kuiacha KNCU ambacho ni kikongwe cha ushirika nchini kutoka moja ya mikoa maarufu kwa ulimaji kahawa.


“Tunataka kujua hao walioteuliwa wanalima nini na kwanini kaskazini tumenyimwa uwakilishi kuna nini?” alihoji.
Makamu Mwenyekiti huyo alisema wanajipanga kujadili suala hilo katika jukwaa la ushirika linalotarajiwa kufanyika hivi karibuni, akisema kaskazini kunyimwa uwakilishi haikubaliki. 


Post a Comment

0 Comments