RAIS DKT. JOHN MAGUFULI AKIWA KATIKA PICHA YA KUMBUKUMBU NA WAZIRI WA MAFUTA NA GESI WA OMAN.
UJUMBE wa serikali ya Oman ambao upo nchini kwa ziara ya siku 10 leo unakwenda Bagamoyo mkoani Pwani kuangalia eneo la ujenzi wa viwanda, ili uwekezaji huo uanze mara moja.
Hatua hiyo ambayo ilielezwa katika taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais ya jana, inaleta matumaini ya kumwagika kwa ajira mbalimbali ndani ya muda mfupi ujao.
Akizungumza Ikulu, jijini Dar es Salaam baada ya majadiliano na Rais John Magufuli, taarifa hiyo ilisema, Waziri wa Mafuta na Gesi wa Oman, Dk. Mohammed Hamad Al Rumhy alisema yeye na ujumbe wake wa watu 300 watakwenda Bagamoyo leo kuangalia eneo la ujenzi wa viwanda, ili kazi hiyo ianze mara moja.
“Mhe. Rais tunataka kushirikiana nanyi kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo," taarifa ya Ikulu ilimkariri Dk. Al Rumhy akisema.
"Tunataka Bagamoyo isiwe eneo la bandari tu, bali pia liwe ni eneo ambalo tutajenga viwanda mbalimbali, tuzalishe mbolea na tununue mazao ya wakulima na kuyasafirisha.
"Sisi tupo tayari na kesho (leo) tunakwenda kuangalia eneo hilo, ili kazi zianze mara moja.”
Taarifa hiyo ilisema zaidi kuwa Dk. Al Rumhy alikuwa akizungumza kwa niaba ya Mfalme wa Oman, Mtukufu Sayyid Qaboos bin Said Al Said.
Mfalme huyo, imeelezwa, alimuahidi Rais Magufuli kuwa nchi hiyo ipo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuongeza uwekezaji katika, pamoja na maeneo mengine, viwanda.
Imeelezwa Oman pia inaunga mkono jitihada za Rais Magufuli za uzalishaji wa nishati, kuongeza thamani ya madini, kuendeleza sekta ya gesi na mafuta na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo, ili kukuza uchumi kwa kasi zaidi.
Ujumbe huo wa Oman ulioanzia ziara yake Zanzibar kwa siku tano kabla ya kuja Bara juzi, una pia Waziri wa Uwekezaji wa Oman, Salem Ben Nasser Al Ismaily, Naibu Waziri wa Utalii, Maitha Saif Majid, maofisa na wafanyabiashara.
Ziara hiyo imelenga kuimarisha uhusiano kati ya Tanzania na Oman hususani katika masuala ya uchumi.
Taarifa ya Ikulu ilisema mbali ya Oman kuahidi kubadilishana uzoefu na Tanzania kuhusu biashara ya mafuta na gesi, itajenga kiwanda kikubwa cha kuzalisha mbolea katika ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo.
Pia, taarifa hiyo ilisema zaidi, Oman itajenga viwanda vya mazao na kununua mazao ya wakulima na itawekeza katika uchakataji wa madini, ili kuongeza thamani.
IPO TAYARI
Kwa upande wake, taarifa ya Ikulu ilisema, Rais Magufuli alimshukuru Mfalme wa Oman kwa kutuma ujumbe huo na kumhakikishia kuwa Tanzania ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Oman.
Rais Magufuli alimtaka Dk. Rumhy, taarifa ya Ikulu ilisema, kufikisha ujumbe wake kwa Mfalme na wawekezaji wa Oman kuwa atafurahi kuona uwekezaji huo unaanza mara moja na kwamba Serikali itatoa ushirikiano wowote utakaohitajika kwa manufaa ya pande zote mbili.
Dk. Rummy, alionekana katika taarifa ya video ya Ikulu akizungumza Kiswahili fasaha.
“Mhe. Dk. Mohamed naomba ukamwambie Mfalme kuwa namshukuru kwa ujumbe huu na namkaribisha sana Tanzania," taarifa ilimkariri Rais Magufuli akisema.
"Nimefurahi kuona mpo tayari kushirikiana nasi kujenga viwanda, kuzalisha mazao na kuendeleza ukanda wa uwekezaji wa Bagamoyo. Sisi tupo tayari hata leo."
"Njooni tushirikiane kwa sababu nyinyi ni ndugu zetu na tutafanya uwekezaji kwa faida yetu sote.”
Aidha, taarifa hiyo ilisema Rais Magufuli ametaka Oman iongeze ushirikiano na Tanzania katika masuala ya utalii na usafiri wa anga, kuwekeza katika usindikaji wa nyama na uvuvi na ushirikiano katika kubadilishana wataalamu wa nyanja mbalimbali wakiwamo walimu wa lugha za Kiswahili na Kiarabu.
Rais Magufuli pia alimshukuru Mfalme wa Oman kwa msaada wa ujenzi wa visima vya maji 100 hapa nchini, taarifa ilisema.
Pia, Rais Magufuli aliiomba Oman kuungana na Serikali katika safari yake ya kuhamia Dodoma kwa kujenga miundombinu itakayoweka kumbukumbu ya ushirikiano wa kindugu na kihistoria kati ya nchi hizi mbili, imeelezwa.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Suzan Kolimba, ilielezwa.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
18 Oktoba, 2017
0 Comments