Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Selemani Jafo amewaagiza wataalam wa sekta ya afya wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kutunza vifaa tiba vilivyotolewa kwa msaada kutoka Taasisi ya Dhi Nurein Foundation.
Taasisi hiyo imesaidia ujenzi wa jengo la dharula, wodi ya wazazi, pamoja na vifaa mbalimbali vya afya ambapo Mradi huo umegharimu zaidi ya Sh.Milioni 900. Hatua hiyo ya taasisi hiyo ni mkombozi mkubwa kwa wananchi wa wilaya ya Bagamoyo na maeneo mengine hapa nchini.
Akizungumza katika uzinduzi wa Mradi huo kwa niaba ya Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Jafo amesema taasisi hiyo inaungana na taasisi zingine hapa nchini zinazosaidia miradi mbalimbali na kuagiza vifaa hivyo kulindwa na kutunzwa bila kupoteza.
Jafo amesema kuna baadhi ya watu wachache hapa nchini wasio waadilifu wamekuwa na tabia ya kuchukua vifaa vizuri vya hospitali na kuvihamishia katika hospitali zao binafsi. Wakati huo huo, Waziri Jafo amewapongeza sana Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, pamoja na Mbunge wa Bagamoyo Shukuru Kawambwa kwa kufanikisha upatikanaji wa mradi huo.
Pia Jafo amewaomba wananchi wajiunge katika mifuko mbalimbali ya bima ya afya ikiwemu CHF iliyo boreshwa ili waweze kupata huduma bora ya matibabu wao na familia zao.
0 Comments