Rais John Magufuli anatarajiwa kuongoza mkutano wa vyama vya siasa vyenye mlengo wa kijamaa utakaofanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 17, mwaka huu.
Mkutano huo pia utashirikisha viongozi wa mataifa mbalimbali akiwamo Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi ambaye atawakilisha Chama cha kikomunisti cha nchi hiyo (CPC).
Wengine watakaoshiriki katika mkutano huo ni viongozi wa vyama vilivyopigania uhuru na ukombozi wa Bara la Afrika na Kusini mwa bara hilo, vikiwamo vyama vya Frelimo, ANC ,ZANU PF na vinginevyo.
Mkutano huo ni wa pili kufanyika Duniani, ambapo wa kwanza ulifanyika Beijing, China Desemba mwaka jana, ambapo Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping alihudhuria na kuziasa nchi za Afrika kuleta maendeleo.
China ni miongoni mwa nchi zilizo mstari wa mbele kusaidia nchi za Afrika ikiwamo Tanzania katika kuhakikisha kuwa nchi hizo zinapiga hatua za kimaendeleo katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii, hali ambayo inaweza kuwasaidia kuondoka kwenye utegemezi.
Miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na China kwa upande wa Tanzania ni pamoja na ujenzi wa reli, barabara na kwenye miradi mingine ya kimaendeleo na kimkakati.
Hivyo basi katika mkutano huo, wadau wataweza kubadilisha mawazo na uzoefu na kujenga taswira mpya ya kimaendeleo kupitia vyama vya siasa na kuandaa mikakati mipya katika utekelezaji wa majukumu yao.
Hata hivyo katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli ataongozana na Waziri Wang Yi kwa ajili ya kuweka jiwe la jiwe la Msingi la ujenzi wa Chuo Cha Uongozi Cha Chama Cha Mapinduzi(CCM) kitakachojengwa Kibaha mkoani Pwani.
Chuo hicho kitaanza kutoa mafunzo mwaka 2020 ambapo, wanafunzi kutoka nchi zilizopigania uhuru na ukombozi wa Bara la Afrika watapata mafunzo.
0 Comments