Serikali Imewataka Wadhibiti Ubora Wa Elimu Kutekeleza Majukumu Yao Kwa Weledi

Serikali Imewataka Wadhibiti Ubora Wa Elimu Kutekeleza Majukumu Yao Kwa Weledi



Frank Mvungi- MAELEZO, Dodoma
Serikali imewataka Wadhibiti Ubora wa Elimu katika ngazi zote kutekeleleza majukumu yao kwa weledi ili kukuza kiwango cha elimu hapa nchini.


Akizungumza leo Jijini Dodoma wakati wa hafla ya kukabidhi magari 47 kwa wadhibiti Ubora wa Elimu na Baraza la Mitihani (NECTA), Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako amesema ku ni utekelezaji wa sehemu ya mikakakti ya kukuza elimu hapa nchini hasa kipindi hiki Taifa linapoelekea katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.


Kati ya hayo, 45 yamekabidhiwa kwa wadhibiti ubora wa elimu ngazi ya Kanda na Wilaya na 2 kwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) .


“Imani yangu ni kuwa magari haya yatatunzwa vizuri na yatatumika kufanya kazi na malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo hivyo yatasaidia kuboresha elimu hapa nchini ” Alisisitiza Prof. Ndalichako


Akifafanua, Prof. Ndalichako amesema kuwa magari hayo yanalenga kusaidia Taifa kuzalisha wataalamu wenye weledi, mahiri na wabunifu hasa katika kipindi hiki Taifa linapoelekea katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.


Aliongeza kuwa Serikali haitasita kuwachukulia hatua kali wale wote watakaotumia magari hayo kwa maslahi binafsi na wale watakaoshindwa kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia sekta ya elimu.


Katika kuimarisha elimu, Prof. Ndalichako amesema kuwa Serikali imefungua ofisi mpya 5 za udhibiti ubora wa shule katika Halmashuri za Songwe, Kigambaoni, Ubungo, Chalinze na Ushetu kwa lengo la kuimarisha shughuli za udhibiti ubora katika Halmashuri.


Jambo jingine ni kuandaliwa kwa mkakati wa Taifa wa Elimu jumuishi (2018-2021) ili kushughulikia masuala ya elimu kwa watoto wote wakiwemo wenye mahitaji maalum na kutoa fursa kwa wadau wengine wa maendeleo kupata maeneo ya kuchangia utekelezaji wa elimu jumuishi.


Hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilikabidhi pikipiki 2,894 ambazo zimesambazwa katika halmashuri 156 katika mikoa 25, pikipiki hizo zitasaidia waratibu elimu kata katika kutekeleza majukumu yao ili kuhakikisha kuwa elimu bora inatolewa shuleni katika maeneo yao.


Magari 45 yaliyotolewa kwa Wadhibiti ubora wa elimu ngazi ya kanda na wilaya na 2 kwa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) ni chachu katika kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini na kuongeza ari kwa watendaji katika sekta ya elimu.

Post a Comment

0 Comments