Waziri Mkuu wa Korea kutua nchini kwa mualiko wa Majaliwa

Waziri Mkuu wa Korea kutua nchini kwa mualiko wa Majaliwa



Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon atafanya ziara ya kikazi nchini kwa mwaliko wa mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), kuanzia tarehe 21 hadi 23 Julai 2018. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kufanywa na kiongozi wa ngazi ya juu kutoka Jamhuri ya Korea tangu nchi zetu mbili zianzishe mahusiano ya kidiplomasia mwaka 1992.

Madhumuni ya ziara hiyo ni kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili na kufungua zaidi fursa za ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi katika ngazi na sekta mbalimbali.

Waziri Mkuu Lee atafuatana na ujumbe mzito wa maafisa wa Serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa. Ujumbe wa wafanyabiashara utakaoongozana na Lee unatarajiwa kukutana na wenzao wa Tanzania katika Mkutano wa Pili wa Jukwaa la Wafanyabiashara uliopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam tarehe 23 Julai 2018. Mkutano wa kwanza ambao ulikuwa na mafanikio makubwa ulifanyika Seoul mwezi Februari 2018.

Lee Nak-yon atawasili nchini saa kumi na mbili na nusu jioni (12:30) ya tarehe 21 Julai 2018 na atapokelewa na mwenyeji wake Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Siku inayofuata, Waziri Mkuu Lee na mwenyeji wake Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.), watafanya mazungumzo rasmi jijini Dar es Salaam na baadaye watashuhudia uwekaji saini wa mkataba wa kuondoa hitaji la visa kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and official/service passport).

Aidha, Lee atakutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa ajili ya kusalimiana.

Jamhuri ya Korea ni mshirika mkubwa wa maendeleo wa Tanzania ambapo kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo (KOICA) na Mfuko wa Ushirikiano wa Uchumi na Maendeleo (EDCF) yamekuwa yakitoa misaada na mikopo mingi ya masharti nafuu kwa Tanzania ikiwemo misaada ya fedha katika bajeti, ujenzi wa miundombinu ya jamii, mafunzo ya muda mfupi na mrefu, wataalamu mbalimbali wa kujitolea, vifaa na mashine kwa ajili ya sekta mbalimbali ikiwemo ya afya.

Baadhi ya miradi ambayo imegharamiwa na Serikali ya Korea ni pamoja na Mradi wa kuboresha Huduma ya Mama na Mtoto katika Hospitali ya Chanika, Mradi wa Mfumo wa Usajili wa Meli na Mabaharia kwa Njia ya Mtandao Zanzibar, Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Taifa ya Taaluma na Tiba (MUHAS) kampasi ya Mloganzila na ujenzi wa daraja katika mto Malagarasi.

Vile vile, Korea ni mshirika mkubwa katika kusaidia maendeleo ya Bara la Afrika ambapo hivi karibuni katika mkutano wa Sita wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na Africa (KOAFEC VI) uliofanyika mwezi Mei 2018, Busan, Korea ambapo Serikali ya Korea ilitangaza msaada wa Dola za Marekani bilioni 5 kwa ajili ya Bara la Afrika kwa kipindi cha mwaka 2018/2020. Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika na msaada huo.

Post a Comment

0 Comments