Jeshi la Polisi mkoani Tabora linawashikilia watu saba kwa tuhuma za kukutwa na zana mbalimbali za kutengeneza noti bandia kwa lengo la kujipatia kipato kwa utapeli.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley alisema watuhumiwa hao walikamatwa Agosti 8, mwaka huu wakati askari wakiwa katika doria.
Aliwataja waliokamatwa kuwa ni Beatus Taita (28) mkazi wa Mwanza, Pasifili Masawe (33), mkazi wa Ipuli, Shaban Mrisho (26) mkazi wa Mwinyi na Anicet Joseph (27) mkazi wa Uzunguni.
Wengine ni Hance Mkonongo (31) mkazi wa Block T Mbeya, Denis Simbee (39) mkazi wa Tunduma na Nickson Shitindi (38) mkazi wa Mbozi, Songwe.
Alieleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na makaratasi yanayotumika kutengeneza noti hizo bandia. Alisema katika mahojiano, watuhumiwa hao walikiri kujihusisha na uhalifu huo.
Katika msako mwingine uliofanyika saa 2.30 usiku siku hiyo polisi walifanikiwa kuwanasa watuhumiwa 12 wa dawa za kulevya katika eneo la Vatican, Kata ya Gongoni Manispaa ya Tabora wakiwa na dawa za kulevya zinazodhaniwa kuwa ni kokeni.
Waliokamatwa ni Khadja Halfan (40), mkazi wa Isevya, Haji Abdallah (45), mkazi wa Isevya, Ally Sunga (23), mkazi wa mkoani, Elias Msuya (29) mkazi wa Ipuli na Yusuph Sijamini (33), mkazi wa Kalunde.
Wengine ni Rashid Mrisho (35), mkazi wa Isevya, Rashid Lungwa (37), mkazi wa Isevya, Gumsan Kairo (28), mkazi wa Isevya, Kulwa Chambi (35), mkazi wa Isevya, Mashaka Akida (25), mkazi wa Isevya, Said Salum (25), mkazi wa Chemchem na Miraji Omar (22), mkazi wa Ipuli.
Alieleza kuwa watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani mara moja baada ya upelelezi kukamilika.
0 Comments