MUONEKANO WA BARABARA ZA JUU KATIKA MAKUTANO YA BARABARA ZA MANDELA NA NYERERE ENEO LA TAZARA.
BARABARA za juu katika makutano ya barabara za Mandela na Nyerere eneo la Tazara wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, zinatarajia kuanza kutumika rasmi Oktoba, mwaka huu.
Meneja wa Wakala wa Barabara (Tanroads) Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamukama, ndiye aliyetangaza tarehe ya kuanza kutumika kwa barabara hizo alipozungumza na Nipashe jijini juzi.
Ndyamukama alisema tayari mradi huo umekamilika, lakini kuna "vitu vidogovidogo" wanamalizia kabla ya kuruhusu barabara kuanza kutumika.
Alisema kuwa kabla ya kutumika rasmi, zitafanyiwa majaribio mwezi ujao ili kujiridhisha na ubora wake.
"Mradi umekamilika, hata wewe ukipita pale utajionea mwenyewe, kazi nzuri na kubwa imefanyika," Ndyamukama alisema.
"Kilichobaki ni 'finishing' (umaliziaji) tu ya vitu vidogo sana kama kufunga taa na vitu vingine vidogo, lakini vitu muhimu vyote vimekamilika.
"Ila kitaalamu tumepanga ifanyiwe majaribio kwanza Septemba na baada ya hapo, Oktoba ianze rasmi kutumika."
Ujenzi wa barabara yenye urefu wa mita 400 umegharimu zaidi ya Sh. bilioni 95.Mradi huo ulianza kutekelezwa mwaka 2016 kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (JICA).
0 Comments