MKUU WA WILAYA YA MUFINDI, JAMUHURI WILLIAM
MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Jamuhuri William, amekifunga kiwanda cha mbao cha Evergreen kilichoko mjini Mafinga kwa siku 14 kutokana na kukiuka sheria na kanuni za usalama kwa wafanyakazi kazini.
William akiwa na timu ya wataalamu mbalimbali kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (Osha), chama cha wafanyakazi (TUICO), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), alifanya ukaguzi na kubaini upungufu na kuagiza kiwanda hicho kifungwe mpaka hapo wataporekebisha kasoro hizo.
Alisema baada ya wataalamu kufanya ukaguzi na kujiridhisha kuwa kiwanda kina upungufu mkubwa wa kutotekeleza maagizo ya serikali na mamlaka zake za usalama wa wafanyakazi kazini, ambao walishatoa kwa kiwanda hicho na kukaidi kuzitekeleza, kiwanda hicho kimepewa wiki mbili kurekebisha mambo hayo.
Mkuu huyo wa wilaya alitaja changamoto za kiwanda hicho kinachomilikiwa na raia wa China kuwa ni pamoja na kukosa mfumo wa uongozi unaoeleweka, ukosefu wa vyoo, maji ya kutosha katika maeneo ya kazi, wafanyakazi kufanya kazi bila vitendea kazi katika mazingira hatarishi kama ukosefu wa viatu maalum, miwani na vifaa vya kuzuia vumbi.
Alisema hivi karibuni, mfanyakazi Omari Chokai (28), ambaye pia ni fundi mitambo, alipigwa na walinzi wa kiwanda wakishirikiana na viongozi kwa madai kuwa mafuta machafu (oil chafu) na alipofika getini walinzi walimuuliza na kusema ameiba kisha kuanza kumpiga kwa kutumia vitu venye ncha kali na kumsababishia maumivu.
Kwa mujibu wa mkuu wa wilaya, baada ya kipigo hicho kijana huyo alizidiwa na kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya Mafinga na alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu. Chokai alifariki dunia Agosti 23, mwaka huu na kupelekwa nyumbani kwao, Konoda mkoani Dodoma kwa mazishi.
Pamoja na tatizo hilo, kiwanda kilishindwa kutoa ushirikiano wa kisafirisha mwili wa marehemu kwa kuzingatia haki ya mfanyakazi anapopata tatizo akiwa kazini.
Kutokana na jambo hilo, mkuu wa wilaya alitoa agizo kwa kiwanda hicho kulipa gharama zote familia ilizotumia kusafirisha mwili na mazishi.
Watuhumiwa watatu walinzi wawili na raia mmoja wa China walikamatwa na polisi na wako mahabusu kwa mahojiano na pindi uchunguzi utakapokamilika watafikishwa mahakamani.
0 Comments