Sheria kuandikwa lugha ya Kiswahili

Sheria kuandikwa lugha ya Kiswahili


Mwanasheria Mkuu wa Serikali, DK. Adelardus Kilangi, amesema ofisi yake iko katika mchakato wa kuanza kuangalia namna ya kuandaa utaratibu wa kutafsiri sheria zote ili zisomeke kwa lugha ya kiswahili.

Kauli hiyo aliitoa jana bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Faida Mohammed Bakar, aliyetaka kujua kama serikali haioni ni wakati mwafaka wa kumuunga mkono Rais kwa kutumia lugha ya Kiswahili hasa katika masuala ya sheria.

"Miswada inaandikwa katika lugha ya Kiingereza, hivyo inatufanya baadhi yetu kushindwa kuchangia vizuri kwani elimu yetu inatofautiana, je, serikali ina mpango gani wa kutafsiri miswada na sheria zetu ili ziwe katika lugha ya kiswahili?" alihoji mbunge huyo.

Akijibu swali hilo, Dk Kilangi alisema ofisi yake itaanza kuandaa utaratibu wa kuhakikisha wanatafsiri sheria zote ili zisomeke kwa lugha ya Kiswahili licha ya kuwa suala hilo linahitaji rasilimali kubwa.

"Suala hili linahitaji rasilimali na utaalamu wa kutosha maana sheria ina utaalamu wake kuitafsiri kutoka kiingereza kwenda Kiswahili vinginevyo itapoteza maana iliyokusudiwa," alisema Dk. Kilangi.

Alisema changamoto waliyo nayo kwa sasa ni uhaba wa wataalam lakini wamejipanga kuyafanyia kazi ili sheria ziandikwe kwa Kiswahili.

Awali, mbunge huyo alitaka kujua ni kwa nini baadhi ya mahakama nchini zinaendeshwa kwa lugha ya Kingereza wakati zinapoendesha mijadala yake katika kutoa hukumu.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu,Kazi,Ajira na Vijana, Anthony Mavunde, alisema mahakama zimekuwa zikitumia Kiswahili na hukumu kuandikwa kwa Kingereza.

"Hali hii inatokana na kuwa Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Madola na inafuata mfumo wa ’Common Law’," alisema Mavunde.

Alisema kwa kuandika hukumu kwa lugha ya Kingereza imewezesha Mahakama ya nchi nyingine za Jumuiya hiyo kutumia hukumu za Tanzania kama rejea na hivyo hivyo Tanzania kutumia hukumu za nchi nyingine.

Mavunde alilihakikishia bunge kuwa sheria,kanuni na taratibu za uendeshaji wa mashauri katika mahakama zetu unaruhusu kutumia lugha zote mbili,Kiswahili na Kingereza na mahakama zimekuwa zikizingatia hilo.

Post a Comment

0 Comments