MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA DK. JANE GOODALL IKULU

MAKAMU WA RAIS AKUTANA NA DK. JANE GOODALL IKULU



Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na Dk. Jane Goodall, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Katika Ujumbe wake Dk. Goodall aliambata na Mama Getrude Mongela na Hadija Simba ambao ni wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Roots and Shoots pamoja na watendaji wengine wa Taasisi hiyo.

Katika mazungumzo yao Dk. Goodall pamoja na mambo mengine amezungumzia uharibifu wa shoroba za wanyama pamoja na makazi yao katika hifadhi ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma ambayo ni maarifu kwa uhifadhi wa Sokwe. Alisema kwa sasa hifadhi hiyo imezungukwa na maakazi ya binadamu hali iliyosababisha kupungua kwa kiasi kikubwa kwa idadi ya wanyama hao.

Aidha Bi. Goodall alimuelezea Makamu wa Rais jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Taasisi yake katika kupambana na uharibifu wa mazingira katika hifadhi ya Gombe ikiwemo kuhimiza uwepo wa mipango bora ya matumizi ya ardhi.

“Inawezekana tatizo kubwa linalosababisha uharibu wa mazingira ni umasikini na uelewa mdogo wa wananchi” alieleza Dk.Goodall. Hata hivyo alisema zipo jitihada mbalimbali zinazochukuliwa na Taasisi yake katika kutoa elimu kwa umma. Kwa sasa wananchi kutoka katika vijiji zaidi 52 mkoani wa Kigoma wanapatiwa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira. Vilevile, jumla ya shilingi Milioni 400 zimekopeshwa kwa wananchi wa vijiji 32 ili kujiwezesha kiuchumi na kushiriki katika miradi ya uhifadhi wa mazingira hususan yenye leno la kulinda shoroba na makazi ya Sokwe. Hali hii imeanza kuleta mafanikio.

Dr. Goodall ametaja changamoto kubwa katika uhifadhi wa mazingira ya Gombe kuwa ni kuwepo kwa wakimbizi kutoka Burundi ambao kwa kiasi kikubwa hushiriki katika shughuli ambazo husababisha uharibu wa mazingira kama vile kilimo na ufugaji usio endelevu.

Kwa upande wake Makamu wa Rais alisema serikali inafanya kazi kubwa katika kuhakikisha mazingira ya hifadhi za taifa pamoja na ikolojia yake yanatunzwa. Makamu wa Rais amemhakikishia Dr. Goodall kwamba serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti ili kuhakiksha wananchi wanafanya shughuli za kujiletea maendeleo bila kuharibu mazingira. “Ni muhimu kuishirikisha jamii inayoishi pembezoni mwa hifadhi zetu katika suala la uhifadhi wa mazingira lakini pia kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi, alisema Makamu wa Rais.

Post a Comment

0 Comments