Nairobi, Kenya. Makamu wa Rais William Ruto amesema hatashiriki mdahalo ulioandaliwa leo kwa ajili ya wagombea wenza kwa madai kwamba hakuwa ameombwa ushauri kwanza kuhusu suala hilo.
Mdahalo wa wagombea wenza kati ya Ruto kutoka Jubilee na Kalonzo Musyoka kutoka muungano wa upinzani (Nasa) ulipangwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki.
"Nimeshangazwa hakuna mtu aliyewasiliana nami kuhusu mdahalo huo. Utaratibu unataka kwamba siku, muda na kanuni zitakazotumika zilipaswa kuwekwa wazi mapema kwa wahusika,” amesema.
Makamu huyo wa Rais ambaye anawania kurudi madarakani, amesema halikuwa jambo la haki kwa yeye kusikia kuhusu mdahalo huo kupitia mitandao ya kijamii badala ya kuambiwa rasmi na waandaaji.
"Ni sawa! Basi sawa, nawatakia kila la heri wale walioshirikishwa. Nadhani kutakuwa na sababu ya kutotendewa haki wote," aliongeza.
Kwa upande wao, waandaaji walisema waliandika barua yenye maelezo kuhusu mdahalo huo na kupeleka ofisi ya Makamu wa Rais.
"Tulimwandikia. Ofisi yake ilipokea barua na ilitiwa saini," alisema Wachira Waruru wa kampuni ya Debates Media.
Mapema, mkurugenzi wa mawasiliano ya kidigitali wa Ikulu, Dennis Itumbi, alisema Makamu wa Rais hatahudhuria.
Badala yake alisema Ruto ataongoza timu ya kampeni katika kaunti za Lamu, Garsen na Kilifi kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Agosti 8.
Hata hivyo, haikufahamika mara moja ikiwa Kalonzo atahudhuria.
0 Comments