Wana CCM 202 wajitokeza kuwania uongozi Kibiti

Wana CCM 202 wajitokeza kuwania uongozi Kibiti


 Wanachama 202 wa CCM wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wilayani hapa, mkoani Pwani.

Akizungumza na gazeti hili, leo Jumatatu Julai 17, Katibu wa CCM wilayani hapa, Zena Mgaya amesema idadi hiyo ni nje ya idadi ya Wana CCM waliochukua fomu za kugombea nafasi za uongozi wa Kata,Shina na Tawi.

Zena amesema pamoja na kuwepo kwa changamoto kubwa za mauaji ya viongozi mbalimbali wa chama hicho, bado mwitikio wa wanachama kuchukua fomu umekuwa wa kuridhisha hasa kuanzia ngazi ya kata na wilaya.

"Pamoja na kuwepo kwa changamoto za mauaji ya mara kwa mara kwa viongozi wetu bado wanachama wetu wamekuwa na mwitikio wa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi," amesema.

Amesema kati ya wanachama waliochukua fomu za kuwani nafasi mbalimbali, 10 wanagombea uongozi kwenye nafasi ya mwenyekiti wa chama hicho ngazi ya wilaya.

Amesema, wanachama wanane wanagombea nafasi ya katibu uenezi na 48 wanagombea nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Wilaya.

“Katika nafasi ya wajumbe wa mkutano mkuu Taifa, wanachama 28 nao wamechukua fomu za kuwania nafasi hizo huku 13 wakiwania uongozi katika nafasi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa mkoa,” amesema na kuongeza:


“Wanachama tisa wanagombea nafasi za uongozi wa Halmashauri Kuu ya Mkoa.”

Amesema katika nafasi za uongozi za Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) ngazi ya wilaya jumla ya wanachama 36 wamechukua fomu kuwania uongozi katika ngazi mbalimbali za jumuiya hiyo.

Wanachama 20 walichukua fomu kugombea nafasi mbalimbali za Jumuiya ya Vijana na 30 wakigombea nafasi mbalimbali kupitia Jumuiya ya Wazazi.

Mmoja wa Wagombea wa nafasi ya uenyekiti, Suleimani Ndumbogani amesema wagombea wote wa nafasi hizo wana ari ya kutaka kuwa viongozi hali inayoleta ushindani mkubwa miongoni mwao.

“Uchaguzi huu upo tofauti na chaguzi nyingine za chama zilizopita kwani wagombea waliokuwa wakigombea nafasi hizo walikuwa wachache tofauti na sasa.” Amesema.

Mmoja wa wanachama wa chama hicho, Rajab Mtwiku amesema uchaguzi huu umekuwa na ushindani licha ya changamoto nyingi za mauaji zilizosababisha wanachama wengi kusita kuchukua fomu.


Post a Comment

0 Comments