Aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Lengai ole Sabaya
Arusha. Aliyekuwa mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Lengai ole Sabaya kwa mara ya nne leo amefutiwa kesi ya kujifanya ofisa usalama wa Taifa.
Sabaya ambaye ni diwani wa Sambasha amefutiwa kesi mbele ya Hakimu Mkazi Nestory Baro wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuwasilisha mashahidi.
Agosti 10, alikamatwa kwa mara ya tatu. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema upelelezi wa shauri lake ulikuwa umekamilika baada ya kesi ya awali kufutwa.
Aprili 28, kesi ya Sabaya iliondolewa mahakamani kutokana na maombi ya upande wa Jamhuri. Alikuwa akidaiwa kutenda kosa la kughushi kitambulisho na kujifanya ofisa usalama wa Taifa.
Hakimu Mkazi, Gwantwa Mwankuga alisema Jamhuri iliomba kesi hiyo iondolewe mahakamani chini ya kifungu cha 91 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Alieleza kusikitishwa na kesi hiyo akisema ilikuwa ni mara ya pili shauri hilo kuondolewa mezani mwake na sababu zikiwa ni zilezile za kukosa mashahidi.
Hakimu Mwankuga alisema kesi namba 376/2016 iliondolewa mahakamani na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) lakini baada ya Mahakama kutoa amri ya kumuachia, lakini alikamatwa na kesi hiyo ilirudi kwake ikiwa na namba 493/2016 ikiwa na mashtaka ya awali.
0 Comments