Mwanasheria wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameikana akaunti ya Twitter (Pichani) iliyoandika maoni kumpongeza mwanamuziki Alikiba
Dar es Salaam. Mwanasheria wa Chadema na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ameikana akaunti ya Twitter iliyoandika maoni kumpongeza mwanamuziki Alikiba, huku ikiwa na picha ya wanamuziki wanaofanya kazi chini ya lebo wa Wasafi.
Lissu amesema hafahamu chochote kuhusu akaunti hiyo na maoni yaliyotolewa akitaka mwandishi amfafanulie.
“Wananisingizia kaka (mhariri wa Mwananchi), ni wimbo gani wa Alikiba?” akimaanisha haelewi chochote kinachoendelea kuhusu uwepo wa wimbo wa “Seduce Me.”
Amesema akaunti hiyo si yake: “Hiyo akaunti ya Twitter si yangu na nilishasema tangu mwaka jana kaka.”
Jana Agosti 29, akaunti hiyo ilikuwa gumzo kwenye mitandao ikiwa imebeba ujumbe unaosema: “Hakuna kitu kibaya kama wanaume sita kuvaa mawigi kupambana na mtu mmoja. #seduceme#.
Tweet hiyo iliambatanishwa na picha ya Kundi la Wasafi wakiwa wamevaa mawigi ambayo waliitoa sambamba na wimbo wao wa “Zilipendwa”.
Mashabiki wanaomuunga mkono Alikiba walifurahi wakiamini kiongozi huyo amejiunga na wengine wengi ambao walijitokeza hadharani kumpongeza Alikiba.
Baadhi ya viongozi waliompongeza Alikiba ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamis Kigwangalla; Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Viti Maalumu, Halima Bulembo.
0 Comments