Askari wakiwa wameimarisha ulinzi nje ya ofisi za wanasheria wa Kampuni ya Immma Advocates zilizopo Mtaa Charambe, Upanga jijini Dar es Salaam zilizoshambuliwa kwa kulipuliwa usiku wa kuamkia Jumamosi ya wiki iliyopita. Polisi imesema jengo hilo limelipuliwa kwa milipuko ya kutengenezwa kienyeji. Picha na Said Khamis
Dar/mikoani. Utekelezaji wa azimio la Baraza la Uongozi la Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kwamba leo na kesho wasusie kwenda mahakamani umewaweka njia panda mawakili.
Rais wa TLS Tundu Lissu, juzi alitangaza uamuzi wa baraza hilo kupinga kushambuliwa kwa ofisi ya mawakili wa kampuni ya Immma, akiwataka mawakili wote nchini kususia kwenda mahakamani leo na kesho.
Alisema baraza hilo limekubaliana kuwa mawakili wote nchini wasiende mahakamani ili kuonyesha kutokubaliana na shambulio hilo lililofanyika usiku wa kuamkia Jumamosi kwenye ofisi hizo Mtaa wa Charambe, Upanga jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi limesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa milipuko iliyotumika katika shambulio hilo imetengenezwa kienyeji.
Mawakili 360 ambao ni wanachama wa TLS mkoani Arusha wanasubiri barua rasmi ya baraza la uongozi la chama hicho ili waitaarifu Mahakama kuhusu uamuzi wa kususia.
Mwenyekiti wa TLS Arusha, Elibariki Maeda alisema jana kuwa ni vigumu kususia kuanzia leo bila kupata barua rasmi ambayo itapelekwa mahakamani.
“Ingawa tunaungana na viongozi wetu kulaani tukio la kushambuliwa ofisi za mawakili wa Immma, lakini tukigoma tu kwenda mahakamani kesho (leo) bila kupeleka barua rasmi, kuna uwezekano wa kuathiri kesi za wateja, ikiwamo kufutwa,” alisema.
Maeda alisema kwa kuzingatia kuwa mawakili wengi ni wa kujitegemea na waajiri wao ni wateja, hivyo kabla ya kugoma wanahitaji kuwa na barua rasmi ambayo ndiyo itafikishwa mahakamani.
“Tumekuwa na vikao leo (jana) na kamati ya uongozi hapa Arusha, tumekubaliana kusubiri barua ya Kamati ya Utendaji (baraza la uongozi) ili tuisambaze kwa wanachama wetu na Mahakama,” alisema.
Wakili mwingine mwanachama wa TLS aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema suala la mgomo linaweza kuwa gumu kutokana na ukweli kuwa kufanya hivyo kutawaathiri wateja wao.
“Mimi siwezi kugoma bila kushauriana na mteja wangu, mfano kesho (leo) nina kesi ina miaka tisa mahakamani sasa nisipoenda ina maana tutapoteza haki ya mteja wangu,” alisema.
Mwenyekiti wa TLS Mwanza, Lenin Njau alisema kimsingi wanaunga mkono azimio hilo, ingawa utekelezaji unasalia kuwa utashi binafsi wa wakili mmojammoja.
“Ingawa kama taasisi tunaunga mkono azimio hilo, suala la kutokwenda mahakamani linabakia kuwa utashi wa mtu mmojammoja,” alisema Njau.
Alisema baadhi ya mawakili wanalaani shambulio hilo na kutaka Serikali na vyombo vya dola kushinikizwa kuharakisha uchunguzi bila kuhusisha mgomo wa kuhudhuria mahakamani na kwenye mabaraza.
Mwenyekiti wa TLS Mkoa wa Dodoma, Steven Kuwayawaya alisema wataendelea na shughuli zao kama kawaida kwa sababu hadi sasa hawajapokea taarifa rasmi. “Hatujapokea official documents (nyaraka rasmi) hadi sasa, kwa hiyo kesho (leo) sisi tutaendelea na shughuli zetu,” alisema.
Ripoti ya uchunguzi wa awali
Wakati wanasheria wakiwa njiapanda, Kaimu Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Benedict Kitalika alizungumza na waandishi wa habari jana na kusema uchunguzi wa awali wa tukio hilo umebaini kuwa milipuko iliyotumika katika shambulizi hilo imetengenezwa kienyeji.
Alisema siku ya tukio, wataalamu walikwenda eneo hilo na walijiridhisha kuwa milipuko hiyo haikutengenezwa viwandani.
Kitalika alisema Agosti 26, jeshi hilo lilibaini kuwa kati ya saa saba na saa nane usiku, watu wasiojulikana utambulisho wao na idadi, walifika ofisi za Immma Advocates wakiwa na magari mawili na walijifanya kuwa askari polisi hivyo kuwarubuni na kuwachukua walinzi wa jengo hilo na kuondoka nao kwenye moja ya gari na walikutwa eneo la Kawe wakiwa hawajitambui.
Alisema kundi lililobaki liliingia ndani ya ofisi hizo na kuweka milipuko iliyotengenezwa kienyeji ambayo baada ya watu hao kuondoka ililipuka na kusababisha uharibifu wa mali, jengo la ofisi na majengo ya jirani.
“Hawa watuhumiwa walijifanya kama ni polisi, hii ilikuwa ni mbinu waliyotumia kufanya uhalifu, hivyo nawaeleza wananchi kuwa walikuwa wahalifu kama wengine si askari kama inavyodaiwa,” alisema.
Kitalika alisema wanaendelea na uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliofanya tukio hili na kujua dhamira yao ili wakamatwe na kufikishwa mbele ya sheria.
Pia, aliwataka waathirika wa tukio hilo na wananchi kwa jumla kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi, hivyo kuwataka wenye taarifa zinazoweza kuwasaidia katika kupeleleza waziwasilishe.
Rais wa TLS, Lissu akizungumza na waandishi wa habari juzi alidai wamepata taarifa kutoka kwa uongozi wa Immma Advocates kuwa kabla ya mlipuko huo polisi wakiwa na magari walifika kwenye ofisi hizo na kuzungumza na walinzi.
Alidai polisi waliwaeleza walinzi kuwa kuna mhalifu ambaye amewatoroka na kuruka uzio ili kuingia ndani ya ofisi hizo, hivyo walikuwa wanataka kuingia ili kumtafuta. Lissu alidai walipoingia, waliwakamata walinzi hao na kuwachoma sindano na baadaye mlipuko huo ukatokea.
Tamko Tume ya Haki za Binadamu
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imetoa tamko kulaani shambulio hilo.
Taarifa iliyotolewa jana na kusainiwa na Mwenyekiti wake, Bahame Nyanduga imesema imesikitishwa na kitendo hicho ambacho kinaashiria uhalifu wenye nia ya kutisha wanasheria wasitekeleze majukumu yao ya kisheria ya kutetea wateja wao.
“Tume inasisitiza kuwa dhana ya utawala bora inategemea utawala wa sheria ambao utaathirika iwapo wanasheria watatishwa na matukio kama ya kupigwa mabomu au vitendo vinginevyo vitakavyowanyima uhuru wa kufanya kazi zao,” inasema taarifa ya tume. Imelitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria.
Pia, imeutaka uongozi wa TLS kusitisha tangazo la kuwataka mawakili kususia vikao vya Mahakama na mabaraza kwa siku mbili.
Imesema mgomo huo hautakuwa na maana kwa vile vyombo vya usalama vimeshaanza kufanya uchunguzi na kwamba utawaathiri zaidi wateja wao ambao hawahusiki na tukio hilo.
Imeandikwa na Mussa Juma, Godfrey Kimani, Jonathan Musa, Sharon Sauwa, Kelvin Matandiko na Pamela Chilongola.
0 Comments