UCHAMBUZI: Polisi msikubali wachache kutuvuruga

UCHAMBUZI: Polisi msikubali wachache kutuvuruga



Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro By Mussa Juma, Mwananchi

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro yuko katika ziara ya kukutana na askari polisi katika mikoa mbalimbali nchini na ujumbe wake mkubwa amekuwa akihimiza utendaji bora wa kazi za polisi.

Katika mikutano hiyo Sirro amekuwa akisisitiza polisi kufanya kazi kwa weledi kwa kutambua kuwa wao ni watumishi wa umma na hivyo wanapaswa kufuata maadili ya utumishi wa umma.

Sirro amekuwa akiwataka askari hao kutenda haki, kuacha tabia ya kubambikia raia kesi lakini pia anawaonya baadhi yao ambao wanakiuka maadili kwa kuwataja watu wanaowapa siri za wahalifu.

Katika ziara hiyo Sirro ameendelea kutoa wito kwa Watanzania kuwataja wahalifu, wakiwamo waliokuwa wanaendesha mauaji katika eneo la Kibiti mkoani Pwani.

Anasema donge nono la Sh10 milioni bado lipo kwa Mtanzania ambaye atafanikisha kukamatwa watuhumiwa waliokimbia pamoja na silaha zao.

Nimerejea maagizo haya ya Sirro kwa kuwa yanaibua matukio ambayo si ya kistaarabu na mageni kwetu.


Matukio haya kama yakiachwa bila wahusika kukemewa na kuchukuliwa hatua, yanaweza kuanza kuendelea na hivyo kuwa tishio kwa Taifa.


Tumeshuhudia yaliyotokea Kibiti na sasa tumeanza kushuhudia mengine ya kuvamiwa ofisi ya wanasheria, wengine kujeruhiwa na wanaodhaniwa majambazi.


Kitendo kilichotokea Agosti 26 cha kulipuliwa ofisi za kampuni ya wanasheria ya Immma zilizopo Mtaa wa Charambe, Upanga jiji Dar es Salaam ni cha kulaaniwa na wapenda haki.


Kimsingi hakuna sababu yoyote inayoweza kuhalalisha tukio hili ambalo si tu limewaathiri wanasheria wa kampuni ya Immma bali ni tishio kwa mawakili wote.


Tukio hili pia linaweza kuhesabika kama moja ya matukio ambayo yanatishia vyombo vya kutetea haki katika jamii na kwa kawaida matukio kama haya huanza taratibu na bila hatua kali kuchukuliwa, yanaweza kuzoeleka na baadaye kusambaa nchi nzima.


Hivi karibuni tumepata taarifa za Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Khalfani Ulaya kuvamiwa, jambo ambalo halijawahi kutokea.


Mapema mwaka huu, tulishuhudia Wakili Shillinde Ngalula ambaye pia ni Mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu (LHRC) Mkoa wa Arusha, akikamatwa na kuhojiwa akiwa anatimiza wajibu wake.

Pia, tumeshuhudia matukio kadhaa ya kunyanyaswa dhidi ya maofisa wa mahakama katika maeneo mbalimbali nchini, hasa wale ambao wanajitokeza kutetea watuhumiwa.

Pia, tumeshuhudia matamko mbalimbali yanayoweza kuathiri uhuru wa mahakama, ambayo hayajawahi kutokea miaka ya nyuma.

Hivyo, kwa muktadha huu, itoshe kuliomba Jeshi la Polisi, kuanza kufanya uchunguzi wa kina kuwabaini watu ambao wanataka kuliyumbisha Taifa na kukemea matendo yote ya kuingilia uhuru wa mahakama.

Kama ambavyo Sirro ameahidi, jeshi hilo litatunza siri za watoa taarifa ili kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu.

Hivyo nitoe wito kwa wananchi wenye taarifa sahihi za wahusika wa tukio hili watoe taarifa polisi ili hatua zichukuliwe, badala ya kuanza kutoa tuhuma mbalimbali zitakazokwamisha mapambano dhidi ya uhalifu huu.

Ni kutokana na umuhimu huo, ndio maana nikasema Jeshi la Polisi lisikubali kuwaacha wachache wavuruge ustaarabu wetu, ambao umekuwa ni wa mfano miaka mingi hata nje ya Afrika.

Post a Comment

0 Comments